Miaka minne iliyopita, waasi nchini Libya walisherehekea kifo cha aliyekuwa rais Muammar Gaddafi.
Bastola yake iliyofunikwa imepambwa kwa dhahabu iliinuliwa juu na wapiganaji hao, ikiwa ishara ya ushindi dhidi ya utawala wa Gaddafi.
Kwa furaha, wapiganaji hao waliipokezana kwa zamu!
Bastola hiyo ilikuwa silaha binafsi ya Gaddafi, japo kwa wakati huo ilibadilika na kuwa ishara ya ushindi kwa waasi, na uhamisho wa mamlaka, katika mwamko mpya wa Libya.
Mjini Misrata, kilomita 200 mashariki mwa mji mkuu wa Tripoli, ndipo inapoaminika kuwa bunduki hiyo ipo kwa sasa.
Mwandishi wa BBC Gabriel Gatehouse alishuhudia sherehe hizo zilizohusisha bastola hiyo moja kwa moja.
Na baada ya miaka minne, Gabriel Gatehouse, amerejea Libya kutafuta bastola hiyo na pia kuona jinsi maisha yalivyo kwa waasi waliomwangamiza Gaddafi.
Anaanza kwa kumtembelea mdokezi wake wa zamani Anwar Suwan.
Alihusika sana katika mapinduzi Misrata. Gaddafi alipouawa, wapiganaji walipeleka mwili wake kwa Anwar, na Anwar akauweka mwili huo hadharani watu wauone, ukiwa umewekwa kwenye jokofu kubwa la kuhifadhia nyama.
Anapomwambia kwamba anamtafuta mtu aliye na bunduki ya Gaddafi, mara moja anamfikiria Omran Shabaan, mmoja wa wapiganaji waliomkamata Gaddafi.
Kwenye kanda ya video iliyopigwa na waasi kwa kutumia simu, Shabaan anasikika akiwasihi watu wasimuue Gaddafi.
Mwingine aliyekuwepo siku hiyo, Ayman Almani, anamwonyesha Gatehouse video aliyoichukua siku hiyo, ambayo haijawahi kuonyeshwa kwenye vyombo vya habari awali.
Inaonyesha nyakati za mwisho za kiongozi huyo wa kiimla, anaonekana akitokwa na damu na kuwasihi watu wasimuue.
Omran Shabaan aligeuka na kuwa shujaa. Alipigwa picha akiwa na video hiyo iliyopambwa kwa dhahabu na akawa ishara ya matumaini kwamba Libya ingejikwamua.
Lakini hili halikuwa na mapigano yameendelea.
Mwaka 2012, Shabaan mwenyewe alikamatwa na wafuasi wa Gaddafi eneo la Bani Walid. Walimpiga na kumtesa. Wapiganaji wa Misrata walipofanikiwa kumkomboa, walikuwa wamechelewa sana. Alifariki kutokana na majeraha akitibiwa hospitali moja Ufaransa.
Anwar Suwan anamwambia Gatehouse kwamba huenda Shabaan alikuwa na bastola hiyo alipokamatwa na wafuasi wa Gaddafi.
Huenda imo mikononi mwa wafuasi hao wa Gaddafi.
Kwenye simu yake ya rununu, Gatehouse ana picha aliyoipiga tarehe 20 Oktoba mwaka 2011 siku ambayo Gaddafi aliuawa.
Ninamuonyesha picha hiyo. Ni picha ya kijana mmoja, akiwa amevalia shati la rangi ya samawati, na kofia ambayo ni maarufu na wachezaji wa mpira wa magongo wa New York Yankees.
“Mohammed Elbibi,” mtu mmoja anamtambua.
Kwenye picha, Mohammed anaonekana akitabasamu huku akibebwa juu kwa juu na wenzake, akiwa ameinua bastola hiyo.
Anwar anasema hajui yaliyomsibu Mohammed lakini anaahidi kusaidia kumtafuta.
Baada ya muda mrefu, Gabriel Gatehouse, alipata anwani yake Mohammed Elbibi, kijana aliyekuwa kwenye picha aliyoipiga akiwa ameinua bastola hiyo.
Alimpigia simu na akakubali kukutana naye.
Anapomwonyesha picha yake, anatabasamu na kusema, "naikumbuka, nilikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo".
"Bunduki unayo?" Gabriel anauliza.
Mohammed angali anaihifadhi bastola hiyo!
Ni bastola ya milimita 9 aina ya Browning, iliyofunikwa kwa safu nyembamba ya dhahabu ikiwa imepambwa kwa miundo ya maua.
Mohammed anasema kamwe hakumuua Gaddafi.
Anasema aliokota bunduki hiyo karibu na mahali ambapo Gaddafi alikamatwa, na katika mtafaruku uliokuwepo, na pia alipoonekana na bastola hiyo, waasi wengine walidhani Mohammed ndiye aliyemuua Gaddafi, na papo hapo akakuwa shujaa wa mapinduzi nchini Libya!
Hata hivyo Mohammed anaishi kwa woga.
Wafuasi wa Gaddafi wanatishia maisha yake.
"Tafadhali elezea ulimwengu kuwa sio mimi niliyemuua Gaddafi," Mohammed anasema.
SOURCE: BBC SWAHILI