MAGUFULI ASIMAMISHA KAZI NA KURUDISHA MABALOZI NCHINI

MAGUFULI ASIMAMISHA KAZI NA KURUDISHA MABALOZI NCHINI

1. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

1.1 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.

1.2 Aidha, baada ya utenguzi huo, Bwana Dickson E. MAIMU amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, pamoja na wafuatao:

1.2.1 Bwana Joseph MAKANI, Mkurugenzi wa TEHAMA
1.2.2. Bi Rahel MAPANDE, Afisa Ugavi Mkuu
1.2.3 Bi Sabrina NYONI, Mkurugenzi wa Sheria
1.2.4 Bwana George NTALIMA, Afisa usafirishaji

1.3 Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

1.4 Hivyo, Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.

1.5 Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.

1.6 Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.

2.0 Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

2.1 Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.

2.2 Rais ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha. Leo hii Mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au Mwandamizi aliye chini yao. Mabalozi hao ni:

2.2.1 Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan

2. 2.2 Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia.

2.3 Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan KALLAGHE. Anarejea Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa atakapopangiwa kazi nyingine.

2.4 Kwa maana hiyo, vituo vya Ubalozi vifuatavyo viko wazi:

2.4.1 London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. KALLAGHE

2.4.2 Brussels, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous KAMALA kuchaguliwa kuwa Mbunge.

2.4.3 Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dkt. James Alex MSEKELA.

2.4.4 Tokyo, Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Bibi Batilda BURIANI

2.4.5 Kuala Lumpar, Malaysia, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Aziz Ponray MLIMA, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.

2.4.6 Brasilia, Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Bwana Francis MALAMBUGI.

3.0 Tawala za Mikoa

3.1 Rais ametengua uteuzi wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.

3.2 Nachukua nafasi hii kuwahimiza viongozi wote katika Utumishi wa Umma, na watumishi wote wa umma, kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu wao.

3.3 Napenda kusisitiza kuwa Rais na sisi tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine. Tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua. Mambo yafuatayo ni muhimu:

4.0 Utumishi wa Umma

4.2.1 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi.

4.2.2 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu asipate kigugumizi kuchukua

hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.

4.2.3 Lazima uongozi na watumishi wa umma wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima. Kwa sababu hiyo:

a) Kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

b) Kwenye kila Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati. Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu. Ikibidi wananchi wafike Ikulu ina maana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.

c) Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.

d) Kila ofisi ya Serikali iwe na utaratibu wa kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo, na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
25 Januari, 2016
 
SIGNATURE

Ada ya Whatsapp Yafutwa



Wamiliki wa app ya mawasiliano ya WhatsApp wamefuta ada ambayo watumizi wake wamekuwa wakitakiwa kulipa kila baada ya mwaka mmoja.
Wamiliki wa huduma hiyo wamekuwa wakiwatoza watu $0.99 kila mwaka baada ya kuitumia kwa mwaka mmoja.
Ada hiyo ilianza kutozwa miaka michache iliyopita lakini kampuni hiyo inasema haijakuwa na manufaa sana.
Taarifa kutoka kwa wamiliki wa WhatsApp inasema: “Watu wengi wanaotumia WhatsApp hawana kadi za benki na wengine huwa na wasiwasi kwamba baada ya mwaka mmoja watazuiwa kuungana tena na marafiki na jamaa.”
“Kwa hivyo, wiki chache zijazo, tutaondoa ada zote tunazotoza wa wanaotumia aina mbalimbali za app yetu na hutatozwa tena pesa ili kutumia WhatsApp.”
Kwa sasa, WhatsApp, ambayo humilikiwa na Facebook, hutumiwa na watu bilioni moja na kampuni hiyo inatumai kuondolewa kwa ada kutavutia watu wengi zaidi.
SOURCE: BBC SWAHILI
PICHA: BBC SWAHILI

Mwanamume mmoja nchini Kenya ameshtakiwa kusambaza picha alizodai ni za wanajeshi wa Kenya waliouawa nchini Somalia akitumia WhatsApp.


Eddy Reuben Illah ameshtakiwa kwa kueneza: “Picha zinazodaiwa kuwa za miili ya maafisa wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF), waliodaiwa kushambuliwa na kuuawa eneo la El-Adde nchini Somalia ukijua kwamba ni za uchochezi na zingesababisha hofu na wasiwasi miongoni mwa raia.”
Anadaiwa kusambaza picha hizo kwenye kundi la watumiaji wa WhatsApp kwa jina A young peoples union (Muungano wa vijana).
Bw Illah amekanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mwandamizi wa Kiambu, mji ulio karibu na Nairobi, Bw Justus Mutuku.
Juhudi za wakili wake Bw Edwin Sifuna kutaka aachiliwe huru kwa dhamana huru zimegonga mwamba na akatakiwa kuweka dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa Sh50,000, gazeti la Daily Nation limeripoti.
Kesi hiyo itatajwa Februari 2 na kuanza kusikilizwa Februari 12.
SOURCE: BBC SWAHILI
PICHA: BBC SWAHILI

Bulaya Amtaka Wasira Mahakamani




By Jesse Mikofu, Mwananchi
Mwanza. Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya amemtaka aliyekuwa mpinzani wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Stephen Wasira (CCM) kuacha kujificha nyuma ya wapigakura, badala yake ajitokeze kortini kupinga ushindi wake.
Kupitia kwa wakili wake, Tundu Lissu, mbunge huyo alidai mbele ya Jaji Ramadhan Mohamed wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuwa, ingawa jina la Wasira halimo kwenye orodha ya wadai, lakini ametajwa kwenye hoja zote za walalamikaji ambao pia wamekiri kwa hati ya kiapo kuwa hoja walizowasilisha mahakamani walizipata kutoka kwake.
Bulaya alikuwa akiwasilisha hoja za pingamizi aliloweka dhidi ya shauri la madai namba moja la mwaka 2015 lililofunguliwa mahakamani hapo na Magambo Masato na wenzake watatu wakiiomba mahakama kutengua matokeo yaliyompa ushindi mbunge huyo aliyekuwa kada wa CCM kabla ya kuhamia Chadema.
“Kwa nini Wasira asijitokeze mwenyewe kuja mahakamani kudai haki yake iliyokiukwa badala ya kujificha nyuma ya wapigakura ambao kimsingi walipata haki yao ya kikatiba ya kupiga kura?” alihoji Lissu.
Wakili huyo alidai maelezo yote kwenye hati ya madai ya walalamikaji hayataji haki yoyote ya mpigakura iliyokiukwa, bali anayedaiwa kunyimwa haki ni Wasira ambaye siyo mmoja wa walalamikaji.
Bulaya anaiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi hayo akidai walalamikaji hawana haki kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi.
Miongoni mwa madai ya msingi ya walalamikaji wanaowakilishwa na mawakili Constantine Mutalemwa na Denis Kahangwa, wanadai Wasira alikataliwa ombi la kuhesabu wala kuhakiki kura.
Walalamikiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bunda Mjini. Uamuzi wa pingamizi hilo utatolewa Januari 25.

SOURCE: GAZETI LA MWANANCHI
PICHA: MWANANCHI 

Masauni aitaka Nida iharakishe vitambulisho




By Bakari Kiango
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni amesema hajaridhishwa na kasi ya usajili wa watu kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa na kuagiza ziongezwe juhudi kutekeleza suala hilo.
Masauni alitoa kauli hiyo jana, alipofanya ziara ya kutembelea makao makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na kuangalia sehemu ya uhakiki, uingizaji wa taarifa na uandaaji wa vitambulisho.
Alisema licha ya Nida kutimiza agizo la Waziri wa wizara hiyo, Charles Kitwanga aliyeitaka kupanga mkakati wa namna itakavyowasajili watu waliofikia umri wa miaka 18, lakini kasi bado ni ndogo kusajili watu ni tofauti ilivyoanza hadi hivi sasa.
“Suala hili limetimiza miaka mitatu. Lakini hadi sasa wamefikia watu milioni sita, idadi hii ni ndogo nahitaji iongezeke zaidi,” alisema Masauni.
Aliitaka Nida kuharakisha usajili wa watu ili kwenda sambamba na agizo la Kitwanga aliyeitaka NIDA kuandikisha watu wasiopungua milioni 15 katika kipindi cha miezi sita.
“Najua mazungumzo yanaendelea vizuri kati yenu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mkipata vifaa 5,000 vitawasaidia kwenye suala hili,” alisema Masauni.
Pia, alitao rai kwa wananchi kutotengeneza vitambulisho nje ya utaratibu uliopangwa na Serikali na kwamba, atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu alisema wakati wanaanza usajili walikuwa na vifaa 226 na kila kimoja kilikuwa kinaandikisha watu 50 kwa siku, hali iliyowawia vigumu kuandikisha watu wengi kwa wakati.
Hata hivyo, Maimu alisema mwezi huu wanatarajia kupokea mashine 5,000 za BVR kutoka NEC ambazo wana imani zitakuwa msaada mkubwa kuharakisha uandikishaji wa vitambulisho.


“Sasa hivi tumeambiwa mashine hizi zipo katika matengenezo baada ya uchaguzi kwisha na yakikamilika tutapewa,” alisema.

SOURCE: Gazeti la Mwananchi Tarehe 16 January,2016.
PICHA: GAZETI LA MWANANCHI

Kategori

Kategori