Masauni aitaka Nida iharakishe vitambulisho




By Bakari Kiango
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni amesema hajaridhishwa na kasi ya usajili wa watu kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa na kuagiza ziongezwe juhudi kutekeleza suala hilo.
Masauni alitoa kauli hiyo jana, alipofanya ziara ya kutembelea makao makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na kuangalia sehemu ya uhakiki, uingizaji wa taarifa na uandaaji wa vitambulisho.
Alisema licha ya Nida kutimiza agizo la Waziri wa wizara hiyo, Charles Kitwanga aliyeitaka kupanga mkakati wa namna itakavyowasajili watu waliofikia umri wa miaka 18, lakini kasi bado ni ndogo kusajili watu ni tofauti ilivyoanza hadi hivi sasa.
“Suala hili limetimiza miaka mitatu. Lakini hadi sasa wamefikia watu milioni sita, idadi hii ni ndogo nahitaji iongezeke zaidi,” alisema Masauni.
Aliitaka Nida kuharakisha usajili wa watu ili kwenda sambamba na agizo la Kitwanga aliyeitaka NIDA kuandikisha watu wasiopungua milioni 15 katika kipindi cha miezi sita.
“Najua mazungumzo yanaendelea vizuri kati yenu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mkipata vifaa 5,000 vitawasaidia kwenye suala hili,” alisema Masauni.
Pia, alitao rai kwa wananchi kutotengeneza vitambulisho nje ya utaratibu uliopangwa na Serikali na kwamba, atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu alisema wakati wanaanza usajili walikuwa na vifaa 226 na kila kimoja kilikuwa kinaandikisha watu 50 kwa siku, hali iliyowawia vigumu kuandikisha watu wengi kwa wakati.
Hata hivyo, Maimu alisema mwezi huu wanatarajia kupokea mashine 5,000 za BVR kutoka NEC ambazo wana imani zitakuwa msaada mkubwa kuharakisha uandikishaji wa vitambulisho.


“Sasa hivi tumeambiwa mashine hizi zipo katika matengenezo baada ya uchaguzi kwisha na yakikamilika tutapewa,” alisema.

SOURCE: Gazeti la Mwananchi Tarehe 16 January,2016.
PICHA: GAZETI LA MWANANCHI


EmoticonEmoticon