TPDC yapewa nguvu kuagiza mafuta ya akiba





Dar es Salaam. Hofu imetanda kuwa endapo Serikali itapitisha mpango mpya kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuleta mafuta ya akiba nchini, bei za mafuta zitafumuka na kuwaumiza Watanzania.
Hiyo inatokana na taarifa kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amepitisha kanuni zinazoruhusu TPDC kuanzisha kitengo cha kuagiza mafuta nje ya utaratibu wa Uingizaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS) na badala yake wataagiza mafuta kwa zabuni.
Mmoja wa wafanyabiashara wa mafuta ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema: “Kwa vyovyote iwavyo, TPDC hawawezi kuingiza mafuta kwa bei ya chini zaidi ya ile ya BPS, hivyo ikiingiza mafuta hayo kwa bei kubwa, itafanya bei za mafuta katika soko la ndani zipande.”
Mfumo huo wa kuleta mafuta ya akiba nchini, unataka mafuta yauzwe kila baada ya siku 30 na habari zaidi zinasema kuwa gharama za uendeshaji wa mfumo huo zitaingizwa kwenye bei za mafuta.
Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, James Andilile alisema kuwa utaratibu wa kuwa na akiba hiyo ya mafuta kwa taifa upo katika nchi zote duniani na kwamba Serikali imeona huu ni wakati mwafaka kufanya hivyo.
“Mafuta haya yatakuwa ni kwa ajili ya nyakati za dharura na kuliwezesha taifa kuendelea na uzalishaji kama kawaida bila kuathirika na mabadiliko ya haraka yanayoweza kuwapo kama mgomo wa nchi wazalishaji au ajali ya meli za mafuta,”alisema Andilile na kuongeza:
“Kwa kuwa mafuta hupungua kadiri yakaavyo, tutakuwa tunayatoa baada ya muda ili kuepuka yasipotee kabisa. Yatauzwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kwa bei ya soko itakayopangwa na wao kwani ndiyo wenye wanadhamana hiyo.”
Alipoulizwa kuwapo kwa mpango wa TPDC kuanza kuagiza mafuta, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alikiri na kusema tayari Bodi ya Wakurugenzi imeruhusu kuanza mchakato ili kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ya namna ya kukokotoa bei ya mafuta hapa nchini kwa kuhusisha gharama za mafuta yatakayoletwa chini ya mfumo wa BPS na yale ya TPDC.
Kaguo alisema kuwa kwa kuanzia, TPDC itaingiza mafuta kiasi tani 30,000 za petroli, tani 14,000 za dizeli na tani 7,000 za mafuta ya ndege. Kuhusu gharama za utunzaji TPDC imefafanua kuwa hapatakuwa na mabadiliko kwa maelezo kuwa hata kampuni zinazochelewa kutoa mafuta yao bandarini hutunzwa na TIPER lakini hakuna mabadiliko yanayotokea pindi yaingizwapo sokoni.

SOURCE MWANANCHI 


EmoticonEmoticon