Dar es Salaam. Hoja ya kutumia sifa ya ujana kama kigezo cha kuwania urais imezidi kupata upinzani baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kusema jambo la muhimu zaidi ni uwezo na uadilifu.
Profesa Lipumba amesema si kila kijana anaweza kuwa kiongozi wa nchi na umri si kigezo pekee cha kupata uongozi, bali uwezo na uadilifu vinastahili kupewa nafasi katika kuchagua mtu anayefaa kuiongoza nchi.
“Miaka 40 si kigezo pekee cha kumwezesha kijana kukabidhiwa jukumu la kuwa rais wa nchi, badala yake anatakiwa awe kijana makini, mtulivu na msikivu,” alisema.
Alisema pamoja na hayo awe kijana ambaye yuko tayari kujitolea, kwani kazi ya siasa inahitaji zaidi moyo wa kujitolea.
Profesa Lipumba alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Mwanasiasa huyo mtaalamu wa uchumi, mbali na sifa ya ujana ambayo kwa siku za karibuni imeibua mjadala, alizitaja sifa tano za uongozi wa juu wa nchi (urais) kuwa ni uadilifu, kuwa dira ya maendeleo, uwezo wa kuhamasisha, kujua matatizo ya watu, kuwaunganisha pamoja na uzalendo.
Akifafanua, alisema rais mwenye dira ya maendeleo pia anatakiwa kuwa na ufahamu wa matatizo yanayolikabili taifa lake na namna gani ya kukabiliana nayo.
“Sifa muhimu ya rais ajaye ni dira ya kuyajua matatizo tuliyonayo na namna gani atakavyofanya kututoa hapa tulipo ili tuweze kwenda mbele. Kwa hiyo, dira ya maendeleo ni muhimu na suala siyo kuwa na dira tu, dira pekee haitoshi. Unatakiwa uweze kuwaeleza wananchi, pia kuwahamasisha ili waweze kukukubali na kisha wakuunge mkono,” alisema.
Alisema kuwa licha ya utajiri wa rasilimali, Taifa linakabiliwa umaskini uliopindukia na kwamba rais au kiongozi mwenye dira anatakiwa kulisaidia taifa kuhakikisha watu wake wanajikwamua kiuchumi.
“Rais ajaye anapaswa ayaelewe vizuri matatizo ya elimu, huduma za afya, ukosefu wa ajira, matumizi mabaya ya rasilimali… haya yakipewa kipaumbele tutakuwa na Taifa lenye neema,” alisema Lipumba.
“Tunahitaji rais mwadilifu ambaye anaweza akasimamia vizuri mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma. Tunahitaji kiongozi anayeweza kufanya kazi na kuwaunganisha Watanzania…. Unajua pamoja na kuwa kwenye vyama, ukiwa na mtazamo au msimamo mkali wa vyama, huwezi kuwaunganisha Watanzania wote. Kwa hiyo, lazima rais awe na uwezo wa kuwaunganisha wote bila kujali itikadi zao,” alisema.
Siasa siyo ajira
SOURCE:MWANANCHI



EmoticonEmoticon