Dodoma. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana ulikuwa gumzo katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini hapa.
Mjadala katika kikao hicho ulijikita kusaka mwafaka na moja ya maazimio yake, ni kuendelea majadiliano ya kusaka maridhiano baina ya chama hicho na vyama vinavyounda Ukawa ili kukwamua mchakato wa Katiba Mpya.
Kamati hiyo ilitoa maelekezo hayo baada ya kupokea na kujadili taarifa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya pamoja na taarifa za mazungumzo ya kusaka maridhiano yaliyofanyika katika ngazi tofauti na kwa nyakati tofauti.
Habari kutoka ndani ya CC iliyofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete ziliyataja mazungumzo hayo kuwa ni yale yaliyowahusisha makatibu wakuu wa vyama, yale yaliyofanyika chini ya uratibu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na yaliyoratibiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
“Kamati Kuu imemwagiza Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) kuendelea na jitihada za mazungumzo tena kwa uzito zaidi, maana sisi (CCM) hatujawahi kukataa mazungumzo na tumeona baadhi ya mapendekezo yao yana maana sana na yana nafasi yake katika mchakato huu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho.
Chanzo chetu kilimnukuu Rais Kikwete akisema kwa kuzingatia mchakato wa Katiba ulivyo, si vyema kupuuza kila kinachosemwa na wapinzani kwani baadhi ya mawazo yao yanaweza kuongeza thamani katika mchakato huo.
Habari zinasema maelekezo ya kuwashawishi Ukawa ili warejee katika meza ya mazungumzo na baadaye bungeni, ni matokeo ya mjadala ulioonyesha kutokuwapo kwa uwezekano wa kupatikana kwa theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Zanzibar wakati wa kupitisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu.
“Baada ya hesabu kupigwa ilionekana kwamba tunahitaji kura 141 kutoka Zanzibar na kwa hesabu za pale kikaoni ilisemekana kwamba tayari tuna kura za uhakika 135, kwa hiyo zinazotafutwa ni kura sita tu,” kilisema chanzo kingine na kuongeza:
“Kutokana na hilo ilikuja hoja kwamba hata kama tungepata hizo kura sita mchakato kwa ujumla wake utakosa uhalali wa kisiasa kwa sababu Ukawa hawamo kwenye kikao na hakuna dalili ya kurudi.”
Kwa mujibu wa habari hizo kulikuwa na mwelekeo unaomsukuma Rais Kikwete kukutana na kundi hilo linaloundwa na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF ili kuona kama wajumbe wake watarejea bungeni.
Hata hivyo, kikao hicho kiliambiwa kwamba Ukawa hawajawahi kuomba kukutana na Rais licha ya kwamba amekuwa tayari wakati wote. Hivyo kikao kilimwagiza Katibu Mkuu Kinana aendelee na jitihada za mazungumzo kwa kuyatilia maanani kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu yaliyojiri kwenye kikao hicho hakuwa tayari kuzungumza na badala yake alisema taarifa rasmi itatolewa leo saa 2:00 asubuhi atakapokutana na waandishi wa habari Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
SOURCE:Mwananchi
EmoticonEmoticon