Mnyika, Mchange wavutana sakata la mauaji
TUHUMA za mauaji ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilibrod Slaa, zimeendelea baada ya Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika na kada wa chama hicho, Habib Mchange kuvutana hadharani.
Hiyo ni siku chache baada ya Mchange kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wa juu wa Chadema wakiwamo Dk. Willibrod Slaa, Freeman Mbowe (mwenyekiti wa chama), Tundu Lissu (mwanasheria) na Mnyika akidai kuwa wanasuka mipango ya mauaji dhidi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza jana katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Star TV, Mchange alizidi kudai kuwa viongozi hao wanasuka mauaji dhidi ya wananchi na akamtaka Mnyika awaombe radhi Watanzania.
“Ninashangazwa Mnyika anashindwa kusema ukweli, kwani tukiwa katika uchaguzi mdogo Igunga alikuja na kuhangaika usiku kucha ili kufukia tindikali iliyomdhuru kada wa CCM, Mussa Tesha kwamba ndani ya Chadema, Slaa, Mbowe na Lissu eti hawatakiwi kuguswa.
“Huu ni uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu ya Chadema ambayo ilibariki mipango mbalimbali ya mauaji, yakiwamo ya Chacha Wangwe na hata matukio ya Morogoro, Iringa na Arusha,” alidai Mchange.
Mchange alitoa matamshi hayo mazito mbele ya Mnyika kuhusu madai yake kwamba viongozi waandamizi wa chama hicho ndiyo mabingwa wa matukio ya ugaidi na utoaji roho za wenzao.
Hata hivyo, mtangazaji wa kipindi hicho alipomhoji Mchange kwa nini madai hayo hakuyapeleka polisi kipindi chote hadi sasa ndiyo anaibuka nayo, kada huyo alisema amefanya hivyo kwa kuchukuliwa maelezo yake polisi na akawataka Mnyika na Mbowe nao wafanye hivyo.
Mchange ambaye ni mwanachama wa Chadema kutoka Wilaya ya Temeke aliwahi kugombea ubunge katika Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani mwaka 2015 na kushindwa.
Alisema viongozi wa Chadema pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, wamekuwa wakitekeleza mambo hayo hasa wanapotofautiana katika msimamo na mitazamo ndani au nje ya chama.
“Dunia nzima inajua watu hawa wameshiriki kwa ukamilifu kumuondoa duniani aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Wangwe. Hii haina ubishi kwamba Mbowe, Slaa na Mnyika walijaribu mara kadhaa kutaka kumuua kwa sumu na kushindwa mpaka walipoweza kumuua kwa ajali ya kutengeneza Julai 28 mwaka 2008 wakimtumia kijana ambaye dunia nzima inamjua,” alidai Mchange.
Wakati kada huyo akirusha makombora hayo, muda wote Mnyika alikuwa mtulivu huku akionyesha a kutabasamu.
Mchange katika kipindi hicho cha Star Tv, alimshangaa Mnyika kukiri kwamba anamfahamu Mallya wakati awali alimkana kutomfahamu kwa namna yoyote.
Mchange alidai baada ya Wangwe kufariki dunia kwa ajali ya gari eneo la Pandambili, Dodoma Julai 28, 2008 usiku Mnyika alizungumza na waandishi wa habari kesho yake na kumkana Deus Mallya akisema Chadema haimtambui.
“Maana yake ni nini? Ni kwamba Mnyika na Chadema walimkana Mallya kimkakati ili kukiondoa chama kwenye ushahidi wa mauaji ya kiongozi wake mkuu msaidizi,” alidai Mchange na kuhoji, “kwa nini Mnyika alimkana Mallya aliyekuwa si tu rafiki yake lakini mshirika wake mkuu kwenye harakati za ujenzi wa chama?”
Alidai baada tu ya tukio hilo, Dk. Slaa alimuagiza Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi aidhinishe malipo na vijana waliohusika wakapelekwa Mwanza na kuhifadhiwa kwenye Hoteli ya Magnum kwa zaidi ya mwaka mmoja, wakiendeshwa na dereva mmoja maarufu wa Chadema ambaye hakumtaja.
Mnyika ajibu mapigo
Akijibu tuhuma hizo, Mnyika alisema madai ya Mchange hayana ukweli ila anachofanya ni kutafuta huruma ya siasa mbele ya Watanzania.
“Suala la madai ya Igunga ya kuhusika kwangu na tindikali, mimi sikuwapo nchini nilikuwa Zambia kama mwangalizi katika uchaguzi mkuu… sasa nahusikaje.
“Ni muda mrefu chama chetu kimekuwa kikihusishwa na madai haya lakini tuliandika barua kwa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete ili aunde tume ya mahakama kuchunguza madai haya ya muda mrefu dhidi ya chama chetu mpaka sasa yupo kimya.
“Mchange anatumiwa na CCM na chama chake cha ACT ili avuruge. Iweje leo hii aje na hoja ya Wangwe au kwa kuwa ni marehemu, si jambo jema kuzungumzia suala la marehemu…nachotaka kusema ni kwamba watawala lazima wajue hawawezi kutusingizia tuhuma za mauaji wakati mikakati hii inafanywa na wao wenyewe,” alisema Mnyika.
Wiki iliyopita madiwani wawili wa Chadema waliokuwa CCM Mkoa wa Shinyanga, waliibua tuhuma hizo wakidai walitumwa waitungue helikopta ‘ iliyokuwa imewabeba viongozi wa chama hicho akiwamo Dk. Slaa.
Diwani wa Kata ya Ngokolo, Sebastian Mzuka na Zakaria Mfuko wa Kata ya Masekelo, walidai kula njama za kumuua Dk. Slaa, zikipangwa na kile walichodai mtandao mpana wa CCM na Serikali yake.
EmoticonEmoticon