WANACHAMA TADEA:SHIBUDA KAUZIWA CHAMA CHETU



Dar es Salaam. Baadhi ya wafuasi wa Chama cha Tanzania Democratic Alliance (Tadea), wameibuka na kuutuhumu uongozi wa chama hicho kwa ‘kukivuruga na kukiuza’ kwa Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwa niaba ya wanachama wenzake, Joachim Mwingira alisema uongozi umeshindwa kukisimamia chama hicho kikamilifu na tayari umepanga kukibadili jina na kuhamisha makao makuu kwenda Mwanza.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tadea, John Chipaka amekana kuuzwa kwa chama hicho na kuongeza kuwa hawatambui wanachama hao, akiwamo Mwingira.
Kadhalika, Shibuda amesema hana mpango wa kukihama Chadema kwenda chama kingine cha kisiasa licha ya kwamba vyama vingi vinamuomba ajiunge navyo.
Mwingira aliyejiita mwasisi wa Tadea, alisema hawamtaki Shibuda katika chama chao kwa kuwa amekuwa mvurugaji wa vyama nchini na kwamba akishaharibu mambo ‘huteleza kama kambale.’
Katika maelezo yake, Chipaka alisema: “Hayo yote ni mambo ya wahuni wa mtaani naomba wakuonyeshe uthibitisho kwamba Tadea imeuzwa na ni kwa kiasi gani? Kuhusu kuhamisha makao makuu, alihoji.. “Kuna sheria gani ya vyama vya siasa inayotaka makao makuu yawe Dar es Salaam pekee?”
Kuhusu suala la Shibuda, Chipaka alisema mwanasiasa huyo ni Mtanzania kama wengine na anayo haki na uhuru wa kuhamia chama chochote cha siasa anachopenda.
“Tadea ni Tadea. Suala la kubadilisha jina ni tactics (mbinu) za kuimarisha chama, sasa hayo yanakujaje kuwa kwenye vyombo vya habari. Ili chama kikue ni lazima kiwe na mbinu… waache kuingilia mambo yetu ya ndani,” alisema Chipaka.
Kwa upande wake, Shibuda aliyeonekana kushtushwa na taarifa hizo, alisema hatima yake ya siasa ipo ndani ya nafsi yake na kwamba hakuna mtu atakayempangia.
“Sijatangaza kuondoka Chadema ila nilichosema ni kwamba sitagombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama. Wao kama wana ushahidi nimekinunua Tadea, wakupe hizo nyaraka na gharama ujiridhishe,” alisema Shibuda.
Awali, Mwingira alisema asilimia kubwa ya wafuasi wa Tadea hawautambui uongozi uliopo madarakani na kwamba wanaomba busara za Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuwaruhusu wafanye taratibu za kujiandaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Alisema walishafungua kesi mahakamani kupinga uongozi na kwamba wanaamini iwapo busara hizo zikifanyika, masuala ya uongozi yatamalizwa nje ya Mahakama.
SOURCE:MWANANCHI


EmoticonEmoticon