Dodoma. Kero za Muungano na taasisi zake zilizotajwa na mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba zimekuwa zikiwatesa wajumbe wa Bunge Maalumu katika mijadala ya rasimu ya Katiba inayoendelea kwenye kamati za chombo hicho.
Miongoni mwa maeneo ambayo yametajwa kusababisha mvutano mkali katika kamati nyingi ni muundo wa Bunge ambao ulitajwa na Jaji Warioba wakati akiwasilisha taarifa ya Tume kuwa una kasoro nyingi ambazo zimesababisha malalamiko kutoka kila upande wa Muungano.
Habari kutoka katika vikao kadhaa vya kamati zinasema baadhi ya wajumbe kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walikuwa wakiamini katika muundo wa serikali tatu pamoja na baadhi wa Kundi la 201, wamesimama kidete wakitaka yafanyike mabadiliko makubwa ya muundo wa Bunge la Muungano.
“Muundo wanaopendekeza ni kuwa na Bunge la ‘tatu ndani ya moja’ kwa maana kwamba Spika anakuwa mmoja, lakini huku ndani kunatolewa fursa za wabunge wa Tanzania Bara kunapokuwa na masuala yao na wale wa Zanzibar wakutane kwa masuala yao na yale ya muungano basi wote tukutane,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Namba Tano.
Ikiwa pendekezo la muundo wa aina hiyo ya Bunge utakubaliwa, majimbo ya Zanzibar yatakuwa na mwakilishi mmoja mmoja, tofauti na sasa ambapo kila jimbo lina mbunge anayeshiriki katika Bunge la Muungano na mwakilishi anayeingia katika Baraza la Wawakilishi.
Watetezi wa muundo huo wanasema pia utajibu kero mbili zilizotajwa na Jaji Warioba ambazo ni wabunge kutoka Zanzibar kushiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya muungano na ile ya sheria zinazopitishwa na Bunge la Muungano kulazimika kupata kibali cha Baraza la Wawakilishi kabla ya kuanza kutumika visiwani humo.
Kwa upande wa wabunge wa CCM wenye msimamo huo, wameujenga katika ahadi waliyopewa na viongozi wao kwamba waunge mkono wazo la kubaki na muundo wa serikali mbili ‘zilizoboreshwa’ hivyo wanataka mabadiliko kadhaa tofauti na wahafidhina ambao wamekuwa wakisimamia muundo wa sasa ubaki kama ulivyo.
“Hawa wakubwa wetu sijui vipi, yaani wanataka kila kitu kibaki kama kilivyokuwa na ikiwa hivyo itakuwa tabu kweli. Ukawa watapata sifa kwamba walichokisema kuwa lengo letu (CCM) ni kubaki na mfumo wa sasa kwa kila kitu itakuwa kweli,” alisema mjumbe mwingine wa Kamati Namba 11.
“Haitakuwa na maana sisi kukaa hapa kwa siku zote halafu tunakuja na yaleyale, lazima hizo serikali mbili zilizoboreshwa zionekane kwa watu, ili watuamini kwamba tulibaki hapa kufanya kazi. La sivyo uamuzi wa kurejea na yaleyale utatuweka pagumu sana hata kwenye uchaguzi ujao wa 2015.”
Kamati ya uongozi
Suala hilo pamoja na mengine kadhaa yaliyowekwa kiporo katika baadhi ya kamati kutokana ugumu wake, yalisababisha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu kukutana kwa siku mbili mfululizo (juzi na jana) kujaribu kuyatafutia ufumbuzi.
Juzi kikao hicho kilikutana kwa saa sita, kuanzia saa 5:00 asubuhi na kuahirishwa saa 11:00 jioni, lakini kutokana na kushindwa kumaliza ajenda zake, kilifanyika tena jana kuanzia saa 5:00 asubuhi. Lakini haikuweza kufahamika kuhusu uamuzi wake wa masuala tata yaliyokuwa yakijadiliwa.
SOURCE:MWANANCHI


EmoticonEmoticon