MKAPA AMPIGIA PINDA KAMPENI KIAINA


Mwanza. Rais mstaafu, Benjamini Mkapa amempigia debe Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kiana akisema ni kiongozi anayekubalika kwa wananchi, hivyo wananchi wamuunge mkono kwenye nafasi yake ya sasa.
Pia, Mkapa amesema uadilifu wa Pinda ndiyo chanzo cha watu kumwamini na kumkubali kutokana na kazi nzuri anayoifanya serikalini, hivyo ni kiongozi mfano wa kuigwa.
Mkapa alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati akihitimisha harambee ya kuchangia fedha za mradi wa Mkapa Fellows kwa ajili ya kusaidia kuboresha sekta ya afya vijijini iliyoendeshwa na Pinda. Harambee hiyo iliandaliwa na Taasisi ya Benjamini William Mkapa HIV/AIDS.
“Naomba niwaambie ndugu zangu, kiongozi mzuri ni yule mwadilifu ambaye anakubalika kwa wananchi, hivyo naomba mumuunge mkono Pinda katika kazi yake ya sasa. Nasema hivi kwa sababu wote mmejionea wenyewe kazi aliyoifanya Waziri Mkuu hapa ni kubwa. Tumefanya harambee na watu wameitikia kumuunga mkono, hivyo ni wazi kwamba anakubalika na kuaminiwa na watu,” Mkapa alisema alipopewa nafasi ya kutoa neno la shukrani katika hafla hiyo.
Kauli hiyo ya Mkapa imekuja siku moja baada ya vyombo vya habari kumtaja Pinda kwamba ni miongoni mwa wanaCCM wanaojipanga kuwania urais kupitia chama hicho.
Habari hizo zimedai kuwa tayari Pinda ameanza kuzungumza na makundi mbalimbali kuhusu nia hiyo, wakiwamo wanaCCM aliokutana nao mjini Mwanza juzi.
Kabla ya kuanza kwa harambee hiyo, Pinda alieleza jinsi alivyooteshwa kuwa harambee ingefanikiwa na ikawa hivyo.
“Sisi watoto wa Kifipa huwa tukioteshwa jambo linakuwa la kweli na mimi usiku huu nilioteshwa kuwa harambee hii itafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kweli imefanikiwa,” alisema Pinda huku akicheka.
Akizungumzia kuhusu uchangiaji fedha kwa ajili ya mradi huo, Pinda alisema licha ya mafanikio makubwa kwenye sekta ya afya, bado kuna changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni maambukizi ya Ukimwi kitaifa kuwa asilimia tano, huku vifo vya kina mama wajawazito kitaifa vikiwa juu kwa kina mama 454 kupoteza maisha kati ya wazazi 100,000.
Alisema Tanzania ina upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia 52, jambo ambalo si la kuridhisha... “Katika Kanda hii (ya Ziwa), asilimia 45 ya wanawake ndiyo wanaojifungua kwenye vituo vya afya na wajawazito 500 hufariki kila mwaka, maambukizi ya Ukimwi ni asilimia 4.8 na upungufu wa watumishi ni asilimia 39, hivyo kuna changamoto kubwa inayotakiwa kufanyiwa kazi,” alisema Pinda.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Dk Ellen Senkoro alisema Kanda ya Ziwa ni moja ya maeneo yaliyonufaika kupitia miradi ya taasisi yake ikiwamo kuajiri watumishi mbalimbali wa kuhudumia miradi yake.
MWANANCHI


EmoticonEmoticon