CHADEMA YAWAACHA POLISI KWENYE MATAA



Dar/Mikoani. Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), ‘kimewaacha polisi kwenye mataa’ katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kutojitokeza kwenye maandamano na kuwaacha askari wakiwa wamejipanga barabarani na maeneo nyeti wakiwasubiri, lakini mjini Bukoba chama hicho kilifanya maandamano.
Mjini Bukoba polisi waliojihami jana walionekana wakizunguka mitaa mbalimbali tayari kupambana na wafuasi wa Chadema, ambao waliwapiga chenga na kuandamana katika Kata ya Kibeta kwa umbali wa takribani kilometa mbili wakiwa na mabango (pichani kulia) bila polisi kuwabaini.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Gilles Muroto alisema walikuwa wamejiandaa kupambana na wafuasi wa Chadema kwa kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku nchi nzima.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Wilaya ya Bukoba, Baraka Vedasto alisema wangeandamana kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Jijini Dar es Salaam, wafuasi 12 wa Chadema walikamatwa katika eneo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa baada ya chama hicho kutaka kufanya maandamano kwa makundi kufika katika ofisi hiyo.
Ulinzi ulikuwa mkali katika eneo hilo na maeneo mengine ya jiji hilo ili kuhakikisha wanakabiliana na wafuasi hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Mary Nzuki alisema wanawashikilia watu hao waliowakamata eneo la ofisi za mkuu wa mkoa wakiwa na mabango. Kati yao, watano ni wanawake na saba wanaume.
“Tunaendelea kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani na tunawaomba wananchi kutii sheria bila shuruti kwani wanachokifanya ni kinyume cha sheria na uvunjifu wa amani,” alisema.
Mbali na eneo hilo, askari kanzu na waliovalia sare wakitumia magari na pikipiki waliimarisha ulinzi maeneo mbalimbali hasa makutano ya Barabara ya Morogoro na Kawawa pamoja na makao makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni. Katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa, askari walikuwa wamesimama katika lango la kuingilia ndani huku wakifanya upekuzi kwa watu waliokuwa wakitaka kuingia.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, “Tupo kazini kwani mpira ni dakika 90,” akimaanisha watahakikisha ulinzi unaimarishwa wakati wote.
Mkoani Mbeya, Kamanda wa Polisi, Ahmed Msangi alisema wafuasi na viongozi Chadema watakaothubutu kuandamana atawafanyia kitu kibaya ambacho hawatakisahau maishani.

Alisema maandamano hayo ni batili na yalipigwa marufuku kwa sababu hayana maana hivyo atakayethubutu kuandamana atakutana na kitu ambacho atakijutia.

“Nasema hivi, watu wenye akili timamu za kuchanganua mambo, wamepeleka kesi mahakamani kupinga mchakato wa Katiba, sasa Chadema kwa nini waingie barabarani kama si kutaka kuleta fujo?
“Chadema wanatuchokoza na ninasema wakithubutu kuandamana … bora nifukuzwe kazi, lakini kitu nitakachowafanyia hawatanisahau maishani mwao.”
Kwa Mkoa wa Mwanza, Chadema kimeitisha maandamano leo licha ya kutopewa kibali walichoomba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Adrian Tizeba alisema walipeleka barua polisi lakini zilikataliwa kupokewa hivyo watawahamasisha wananchi kuingia barabarani kuandamana.
Mkoani Singida, maandamano yaliyopangwa kufanyika jana yaligonga mwamba baada ya polisi kutanda katika kila barabara ambazo zingetumika.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Kelvin Matandiko(Dar), Phinias Bashaya (Bukoba), Godfrey Kahango (Mbeya), Jesse Mikofu (Mwanza) na Gasper Andrew (Singida

source mwananchi jumamosi


EmoticonEmoticon