Arusha. Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) limo kwenye harakati za uchaguzi wa viongozi wake na tayari uchukuaji wa fomu umeanza.
Wapo vijana wengi ambao wameanza kutajwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho kuchukua nafasi ya uongozi unaomaliza muda wake, chini ya mwenyekiti wao, John Heche.
Orodha ni ndefu, lakini mmoja wa waliotajwa ni kada maarufu wa Chadema, Godlisten Malisa.
Malisa aliwahi kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza, 2012 / 2013.
Katika mitandao ya kijamii jina la kijana huyu limekuwa likitajwa na katika mtandao wa Jamii Forum kulikuwa na mjadala wenye kichwa cha habari kisemacho: “Nitamuunga mkono Malisa akigombea Bavicha’.
Hali hii ilifanya gazeti hili kumtafuta Malisa na kutaka kujua ni nani na kama kweli ana mipango ya kugombea uongozi ndani ya Bavicha, lakini kwa ufupi alisema hilo siyo moja ya mipango yake ya kisiasa.
Badala yake, Malisa anatamani kuwa meya wa manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ifikapo 2015.
Mahojiani kati ya Malisa na gazeti hili yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwananchi: Umefahamika kama kada maarufu wa Chadema. Je, unaweza kuelezea historia yako kwa kifupi ndani ya chama?
Malisa: Nilijiunga na Chadema 2007 nikiwa bado mwanafunzi wa sekondari. Mwaka 2009 nilichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya ya Moshi nikiwakilisha kata ya Kiborloni.
Mwaka 2011 nilichaguliwa katibu mwenezi wa Chadema Tawi la SAUT nafasi iliyonifanya nikashinda kwa kishindo urais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo mwaka uliofuata.
Mwananchi: Umesema ulipokuwa katibu mwenezi wa Chadema SAUT ilikusaidia kushinda urais wa chuo. Kivipi?
Malisa: Ni kutokana na kazi kubwa niliyoifanya ndani ya chama, ikanijengea jina na heshima kwa jamii ya wana-SAUT na hivyo kuniunga mkono nilipoamua kutangaza nia ya urais mwaka 2012.
Nilishirikiana na viongozi wengine kufanya mambo mengi sana ndani na nje ya tawi. Tulikabidhiwa tawi tukiwa hatuna ofisi, lakini tuliweza kupanga ofisi na kununua vifaa vyote muhimu kwa kutumia michango ya wanachama.
Tuliweza kuongeza idadi ya wanachama kutoka chini ya 100 hadi wanachama zaidi 1,000 mwaka 2011 na 2012. Tuliweza kuanzisha akaunti Benki ya CRDB na kuhifadhi fedha za tawi. Tuliweza pia kuanzisha blogu ya tawi (www.chadema-saut.blogspot.com) ambapo tuliitumia kupeana taarifa mbalimbali za maendeleo ya tawi.
Mwananchi: Unazungumziaje mchakato wa uchaguzi ndani ya Bavicha unaoendelea kwa sasa?
Malisa: Ni utaratibu wa kidemokrasia uliowekwa ndani ya chama ili kupata viongozi wanaoweza kukisaidia chama katika maeneo mbalimbali na kukiwezesha kufikia malengo ambayo ni kumkomboa Mtanzania kutoka mikononi mwa wakoloni weusi.
Mwananchi: Umekuwa mmoja wa watu wanaotajwa sana kuwania nafasi za juu katika umoja huo. Je, una mpango wa kugombea? Kama ndio je ni nafasi gani?
Malisa: Kwanza, mimi kutajwa kugombea Bavicha hakujaanza leo, kwa muda mrefu watu mbalimbali wamenisihi kugombea. Lakini, ukweli ni kwamba “sigombei” Nina sababu mbili za kutogombea mwaka huu.
Mosi, kazi yangu nayofanya kwa sasa hairuhusu kufanya siasa za vyama, pili umri unaniruhusu kugombea miaka mitano ijayo (kwa mujibu wa katiba). Hivyo, nimeona kwa sasa nifanye kazi kwanza na kujipanga kimaisha na ikiwa nitajisikia kuitumikia Chadema ndani ya Bavicha hapo baadaye, basi nitagombea 2019, vinginevyo nitaitumikia chama katika ngazi nyingine.
Mwananchi: Watu wengi walikufahamu ukiwa rais wa SAUT, Je , unadhani ni kwa sababu ulikuwa kada wa Chadema?
Malisa: Hiyo ni mojawapo ya sababu, maana nilikuwa rais wa kwanza na wa mwisho (hadi sasa) niliyekuwa kada wa Chadema na sikuficha hilo. Pili, ni kutokana na mafanikio ya uongozi wa serikali yangu na aliyekuwa makamu wangu, Consolata Michael.
Mwananchi; Je, unafikiri Chadema kushindwa kuwa na rais wake SAUT ni sababu kuwa Chadema imekufa chuoni hapo?.
Malisa: Hapana si kweli, Chadema bado inafanya vizuri, ninachoweza kusema tamaa ndio inayowaangamiza vijana kwakutaka kufika mbali kiraisi.
SOURCE MWANANCHI
EmoticonEmoticon