Dar es Salaam. Mahakama
ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kifungo cha miaka sita jela, Melkiad
Kabunduguru(28) baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia
ya udanganyifu na kukutwa na noti bandia.
Kabunduguru ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Dodoma(Udom) atatumikia kifungo hicho baada ya Mahakama kuridhika na
ushahidi uliotolewa dhidi yake.
Katika shtaka la kwanza la Kabunduguru atatumikia
kifungo cha miaka minne baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha
kwa njia ya udanganyifu huku shtaka la pili la kukutwa na noti 50 za
bandia za Sh5000 mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Juma Hassani
alisema mshtakiwa atatumikia vifungo hivyo kwa pamoja baada ya Mahakama
kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Juma Hassani
alidai kuwa mshtakiwa huyo atatumikia kifungo hicho ili iwe fundisho kwa
vijana wengine wenye tabia za wizi.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, upande wa Jamhuri
ukiongozwa na Mwendesha mashtaka, Felista Mosha uliiomba mahakama kutoa
adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye
tabia za udanganyifu.
“Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama hii tukufu
kutoa adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa huyu kutokana na kushamiri kwa
vitendo vya udanganyifu na kujihusisha na matumizi ya noti bandia wakati
akijua kuwa ni kosa la kisheria,” alidai Mosha .
Baada ya Hakimu Hassani kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, alimuhukumu Mwiganyi kifungo cha miaka sita jela.
Awali, Wakili wa Serikali, Felista Mosha alidai
mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 29, mwaka huu
katika Barabara la Ally Hassan Mwinyi katika mashine ya kutolea fedha
(ATM) ya NMB iliyopo Chuo cha Biashara (CBE) na kujipatia Sh100,000
kutoka kwa Expedith Mtisi kwa madai kuwa angemrejeshea lakini hakufanya
hivyo.
Katika shtaka la pili, mshtakiwa alikutwa na noti bandia 50 za Sh5000.
SOURCE KWA HISANI YA MWANANCHI JUMAMOSI
SOURCE KWA HISANI YA MWANANCHI JUMAMOSI
EmoticonEmoticon