MAANDAMANO YA UKAWA YAPINGWA

Na Khamis Amani
Katiba bora yenye maslahi kwa pande zote mbili za Muungano haitaweza kupatikana kwa maandamano yenye kuashiria uvunjifu wa amani.

Diwani wa wadi ya Kwahani wilaya ya mjini Unguja, Machano Mwadini Omar, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, juu ya mchakato wa katiba mpya unaoendelea.

Alisema wananchi wanapaswa kufahamu lengo la mchakato wa katiba unaoendelea ni kupatikana katiba itakayosimamia mwenendo wa serikali zote mbili zilizounda Muungano.

Alisema upatikanaji wa katiba hiyo utaondosha malalamiko kutokana na kila upande kupata fursa sawa zitakazosimamia kuendesha serikali zao na wananchi wake kwa ujumla kwa misingi ya haki na usawa.


Alisema, katiba hiyo haiwezi kupatikana nje ya vikao vya Bunge Maalumu kwa kuitisha maandamano.

Alisema, kitendo cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge maalumu na kuitisha maandano sio cha busara, kwani hali hiyo haiwezi kusaidia kupata katiba.


Alisema, wajumbe wa Bunge Maalumu ni wawakilishi wa wananchi katika majimbo na makundi yao, hivyo ni vyema kutumia fursa hiyo kuwaitikia na kuwawakilisha ipasavyo wananchi hao ili waweze kupata katiba itakayosimamia haki zao kwa mujibu wa sheria.


EmoticonEmoticon