CAG ATAKA UHURU WA OFISI YAKE



Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh
amewataka wafanyakazi wa ofisi hiyo kuhakikisha Katiba ya nchi inaimarisha na kutunza uhuru
utendaji wa ofisi hiyo.
Utouh ambaye anastaafu wadhifa huo baada ya kutimiza umri wa miaka 65, alisema hayo katika
 hafla ya kumuaga iliyofanyika juzi mjini Dodoma ambapo alionya kuwa bila kuwa na uhuru huo
katika utendaji, huenda mambo yasiende kama inavyotarajiwa.

“Hakikisheni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaimarisha na kutunza uhuru wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,” alisema CAG Utouh huku akiwataka wakaguzi wajipange kwa kusoma zaidi na kuwa wabunifu hasa kipindi hiki ambapo nyanja hiyo inapanuka na kubadilika kwa kasi hasa kipindi hiki ambacho gesi imegundulika huku utafiti
kuhusu mafuta ukiendelea

“Nyanja ya ukaguzi inabadilika, kuna ukaguzi unaotakiwa ufanywe katika miradi ya gesi, mafuta, mazingira, menejimenti na fani nyingine ambazo ni mpya,” alisema na kuongeza: “Yote hayo msingi wake ni kusoma kwa bidii na siyo kubweteka.”

Akizungumzia historia ya ofisi hiyo, Utouh alisema kuwa alipoingia kwenye ofisi hiyo aliikuta inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa wafanyakazi na kwamba katika miaka minane wameongezeka kutoka 493 hadia 814, ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 65.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimsifu CAG kwa kuimarisha miundombinu ya kiutendai hali ambayo iliongeza idadi ya wahasibu na kuifanya Serikali kutafuta miundo na mifumo katika ngazi ya kimataifa.

“Hongera…, umesaidia kuongezeka kwa weledi wa kiuongozi na kiutendaji serikalini, mifumo ya kiutendaji, uwazi na upatikanaji kwa urahisi wa taarifa za msingi kwa jamii sanjari na ushirikishwaji wa wananchi ambao sasa ni mkubwa tofauti na awali,” alisema Makinda

SOURCE GAZETI LA MWANANCHI


EmoticonEmoticon