Wakati joto la uchaguzi 2015 likiendelea kupanda nchini, propaganda za kuwachafua wapinzani zinazidi kuongezeka.
Viongozi wa Serikali ya CCM wanaendelea kukitetea chama chao kwa kila njia.
Mbinu inayoonekana kutumiwa chama hicho tawala ili kushinda uchaguzi ni propaganda katika vyombo vya habari na matumizi mabaya ya dini.
Gazeti la moja wiki iliyopita liliandika habari yenye maneno ya kufuru likimnukuu mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira wakati akimsimika kamanda wa vijana Kata ya Butimba.
Wasira alinukuliwa akisema kwamba upinzani mamlaka yao ni ya kishetani na kwamba CCM mamlaka yao ni ya kutoka kwa Mungu aliye mbinguni.”
Najiuliza je, Wasira anamfahamu shetani au anamsikia? Je, Wasira anamjua Mungu kweli na sifa za Mungu anazijua hadi atamke hivyo? Je, anazijua mamlaka hizi mbili vizuri?
Hii inaonyesha wazi kwamba CCM wanayo ile dhana kuwa “Kikwete ni chaguao la Mungu” na hivi chama chao ni chaguo la Mungu pia.
Niliposoma habari hiyo nilitafakari sana na nikahitimisha kwa kusema kwamba baadhi ya watu ndani ya CCM wanaendelea na mchezo wao wa kumkufuru Mungu aliye juu mbinguni kwa mithili ya mnara wa Babel.
Nikiwa natafakari kauli ile ya Wasira, nikakumbuka mahubiri ya padre mmoja alikuwa anahubiri juu ya shetani kanisani na akawauliza waumini wake: “Je, nani anamjua shetani, nani amewahi kumwona na kama umewahi kumwona tuambie anafananaje?”
Baada ya dakika kama tatu kupita kanisa lote lilikuwa kimya kabisa kama vile ni malaika anapita. Wale waliokaa mbele walikuwa wanainama wasije wakagongana macho na padre na kuwaambia waeleze.
Padre aliamua kurudia swali lake, lakini hakuna aliyejitokeza kujaribu kumjibu. Kwa nini waumini wote waliogopa kumjibu padre swali hili?
Padre aliamua kutoa jibu mwenyewe na akasema “Shetani pia ni mimi na wewe, kwa matendo yetu maovu.” Padre hakumwonyesha muumini yeyote kama ni shetani hata kama anajua kuna watu wanatabia za kishetani.
Ni kwa mantiki hii, najaribu kujiuliza hivi Wasira anamjua shetani au anamsikia tu? Anatumia kigezo gani kuutamka ushetani wa wapinzani?
Vitabu vitakatifu vinatufundisha kuondoa kwanza boriti katika macho yetu ndipo tuweze kuona kibanzi kwa mwingine. Siasa si matusi, kejeli, utekaji, wala ugomvi, vita na mauaji la hasha!
Lakini huko tunakoelekea hasa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kuna kila dalili za nchi ya Tanzania kukosekana kwa utulivu endapo siasa za kibabe zitaendelea kushabikiwa.
Kuwaita wapinzani mashetani ni kuonyesha upeo mdogo wa kujenga hoja na hivyo kutaka kutumia mafundisho ya dini kufanya siasa chafu.
Haya ni matumizi mabaya ya elimu ya imani na huku ni kuvuka mipaka iliyopitiliza.
Kama CCM ina mamlaka kutoka juu kwa Mungu, kwa nini Tanzania kuna matatizo mengi sasa.
Kwa nini albino wanauawa kila siku, mabilioni ya fedha yanaibwa na watu wanaofahamika lakini mamlaka ipo tu, ajali za barabarani ndiyo hizo, mauaji ya kisiasa yamejaa nchini, uvunjaji wa haki za binadamu ni kitu cha kawaida, wizi wa tembo na wanyamapori, mauaji ya raia wasio na hatia, uchomaji wa nyumba za ibada na uchakachuaji wa mchakato wa Katiba, je, hayo ndiyo mamlaka ya kutoka kwa Mungu?
Ni wazi Wasira anajaribu kufanya propaganda (porojo za kisiasa) kuwadanganya Watanzania wasiojua neno la Mungu na maana halisi ya shetani.
Kati ya wapinzani na CCM ni chama gani kina mambo yanayokwenda kinyume na matarajio ya wengi? Kuvuruga maoni na mawazo ya wananchi wa Tanzania na kubandika mawazo yao katika Katiba Mpya je, hilo si jambo la kishetani?
Kwa sababu kuna usemi usemao sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Wasira haoni hapa anapingana na mamlaka ya Mungu ambaye ni Mungu wa watu wote na hasa wale maskini, wanyonge wasiokuwa na sauti?
Ndiyo maana nauliza hivi, Wasira anamjua shetani au anamsikia?
Watanzania wa leo hawawezi kuendelea kudanganywa tena na wanasiasa, huu ni muda wa mabadaliko ambayo hakuna nguvu itakayoweza kuzuia mabadiliko hayo.
Kuonyesha hali ya kutoijua demokrasia na utawala bora Wasira alinukuliwa akisema CCM itahakikisha wapinzani hawapati nafasi ya kutawala Tanzania.
Mungu halazimishi mipango yake kamwe na wala Mungu halewi madaraka na kutumia ubabe na vitisho kama inavyofanya na baadhi ya wanasiasa. Bali, shetani huwa anatumia mbinu chafu, hila, fitina, mauaji, uongo, vitisho, jeuri ili kumtawala mwanadamu.
Baadhi ya watawala hawajali maisha ya wananchi. Wanachojali ni wao kuendelea kuwatawala wananchi maskini na wanyonge na waoga wakisifiwa kwa kigezo cha kuwa ni watiifu na wapenda amani.
Kumbukeni mtu mwenye mamlaka ya Mungu ana heshimu wanadamu, lakini baadhi ya watawala hawana heshima kwa Watanzania. Ushahidi ni jinsi ilivyochakachua maoni ya wananchi ya Rasimu ya Warioba.
Mamlaka ya kutunga Katiba Mpya kama ni sehemu ya Mamlaka ya Mungu kama anavyojigamba Wasira, basi Mungu huyo ni wa kuchongwa na siyo Mungu kama tunavyomjua yaani mpole, mwenye huruma, mtenda haki, mpenda maskini na kadhalika.
Baadhi ya watawala waache kutumia maneno ya Mungu kuhalalisha ulevi wa madaraka kwa sababu Mungu atakapogeuza kibao hamtasalimika.
Mungu hapendi utawala wa mabavu na vitisho kama wanavyofanya baadhi yao.
SOURCE Mwananchi
EmoticonEmoticon