IPTL YAMKABA KOO KAFULILA




Dar es Salaam. Sakata la tuhuma za wizi wa pesa katika Akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT) sasa limehamia mahakamani baada ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kumfungulia mashtaka Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila.
Kafulila amefunguliwa kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na IPTL kwa kushirikiana na Kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited (mlalamikaji wa pili) na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hizo, Harbinder Sigh Seth (mlalamikaji wa tatu).
Katika kesi hiyo namba 131 ya mwaka 2014, walalamikaji kwa pamoja wanaiomba mahakama imwamuru mbunge huyo awalipe fidia ya jumla ya Sh310 bilioni kwa madai ya kutoa kashfa dhidi yao kwa kuwatuhumu kujipatia pesa kutoka Akaunti ya Escrow, kwa njia zisizo halali.
Kwa nyakati tofauti ndani na nje ya Bunge, Kafulila amekuwa akiituhumu PAP na Seth kuchota Sh200 biloni kutoka akaunti hiyo kupitia IPTL isivyo halali, huku pia akiwataja mawaziri na maofisa wengine wa serikalini kuhusika katika wizi huo.
Maombi ya walalamikaji
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo, walalamikaji wanaiomba mahakama imwamuru mbunge huyo awalipe Sh210 bilioni kama fidia kutokana na kashfa hizo na hasara ya taswira ya biashara na hadhi yao.
Pia wanaiomba mahakama imwamuru mdaiwa awalipe Sh100 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na usumbufu walioupata kutokana na taarifa za kashfa zilizotolewa na mdaiwa dhidi yao.
Mbali na malipo hayo ya fidia, pia walalamikaji hao wanaiomba mahakama imwamuru mdaiwa awaombe radhi kutokana na taarifa hizo.
Maombi mengine ni gharama za kesi, riba kwa kiasi cha pesa yote wanayodai kwa kiwango cha asilimia cha mahakama, kutoka tarehe ya hukumu hadi tarehe ya mwisho wa malipo hayo na amri nyingine ambazo mahakama itaona zinafaa.
Inaeleza kuwa kutokana na mgogoro huo, kiasi cha Sh200 bilioni ziliwekwa katika Akaunti ya Escrow iliyofunguliwa BoT, kusubiri kumalizika kwa mgogoro wao huo uliokuwa mahakamani hapo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa mgogoro huo ulimalizika na kuhitimishwa kwa mdai wa kwanza (IPTL) kupata amri ya mahakama kumiliki pesa hizo na BoT kutakiwa kuziachia.
Hati hiyo inaeleza kuwa katika hali ya kushangaza na pasipo na uhalali wowote, madaiwa katika matukio tofautofauti na nje ya Bunge aliamua kusambaza kwenye mitandao ya kijamii taarifa za kashfa dhidi ya mdai wa kwanza na mdai wa tatu.
Mitandao hiyo ya kijamii iliyotumika kusambaza kashfa hizo kwa mujibu wa hati ya madai, ni Jamii Forum, Twitter Facebook.
Hati hiyo ya madai inaeleza kuwa Juni, 2014, mdaiwa alichapisha kuwa mdai wa kwanza na wa tatu walijipatia pesa kutoka akaunti ya Escrow isivyo halali, wakati si kweli.
“Mdaiwa bila uhalali wowote alisambaza taarifa kuwa, mdai wa kwanza amehusika katika vitendo viovu vya kuchukua pesa hizo katika akaunti ya Escrow, jambo ambalo halina ukweli,” ilisomeka hati hiyo.
Pia inadai kuwa mdaiwa amekuwa akitoa taarifa za kashfa huku akimtaja mdai wa tatu kuwa ni Singasinga, jambo ambalo si sawa na hivyo kuharibu sifa yake na kusababisha uendeshaji wa biashara zake zinazotekelezwa na mdai wa kwanza na wa pili kudorora.
Hati hiyo ya madai inaeleza kuwa kitendo cha mdaiwa kutoa taarifa hizo za kashfa kimesabisha jamii kwa jumla kuamini kuwa kweli mdai wa kwanza amejipatia pesa hizo kutoka katika akaunti hiyo isivyo halali na kwamba raslimali zao zinahujumiwa na mdai wa kwanza.
“Zaidi kitendo cha mdaiwa kutangaza kwa jamii taarifa za mdai wa kwanza kujihusisha na mchezo mchafu kimesabisha hasara au kupungua kwa hadhi ya mdai wa kwanza na wa pili.”, inabainisha hati hiyo ya madai.
Inaendelea kueleza kuwa mdaiwa akiwa ni mbunge ana kinga ya kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa yale aliyoayasema bungeni, lakini pia inabainisha kuwa taarifa hizo za kashfa zimesambazwa na mdaiwa nje ya bunge.
Hati hiyo ya madai inaisisitiza kuwa kitendo cha mdaiwa kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwa jamii si tu kwamba kimeshusha hadi ya mdai bali pia kimesabisha hasara ya kibiashara.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, mdaiwa bado anaendelea kutangaza taarifa hizo za kashfa dhidi ya wadai, licha ya taarifa ya maneno nay a maandishi aliyopewa, hivyo kusabaisha hadhi ya wadai kuendelea kushuka na kusabisha hasara ya kibiashara.
Inadai katika hati hiyo kuwa hadhi yao si tu kwamba imeshuka nchini bali pia kimataifa na hivyo kuwasabishia hasara kibiashara, na kwamba taarifa hizo pia zimewasababishia madhara ya kisaikolojia na usumbufu kwa menejimenti nzima.
Inaeleza kuwa kitendo cha mdaiwa kuelezea mambo yaliyojiri katika mahakama za kisheria katika maombi baina ya mdai wa kwanza na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kimesabaisha si tu kuingilia uhuru wa mahakama bali pia hasara kwa mdai wa kwanza.
Wadai wanaendelea kueleza kuwa mdaiwa alikuwa akijua kilichoendelea mahakani katika maombi hayo baina ya mdaiwa wa kwanza na VIP, lakini aliamua kutangaza kinyume kuhusu akaunti ya Escrow.
Hati hiyo inasisitiza kuwa mdai wa kwanza alipata pesa hizo kutokana na amri halali ya mahakama baada ya uamuzi wa maombi hayo baina yake (IPTL) na VIP.
Inaendelea hati hiyo kudai kuwa kwa kuwa mdaiwa wa kwanza anatoa huduma ya kulisambia Tanesco umeme, taarifa hizo za mdaiwa zimejhatarisha uhusiano baina yake (mdai) na Tanesco na hivyo kusabaisha kudorora kwa uchumi na biasha ya wadai.
Alichokisema Kafulila Bungeni
Akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15, Kafulila alisema fedha hizo zilichotwa na Kamapuni ya Pan African Power Solutions (PAP).
Alisema kuwa kampuni hiyo ambayo iliidhinishiwa kuchota fedha hizo kinyume na utaratibu kwa ya “Singasinga na kwamba ni ya kitapeli.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo iliidhinishiwa pesa hizo kwa udanganyifu mkubwa kwamba PAP ilikuwa imenunua IPTL wakati jambo hilo sio la kweli.
Mbali na Kampuni hiyo aliwahusisha Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu wake na pia Waziri wa Fedha, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na vigogo wengine wa BoT na wa serikalini.
Mbunge huyo alisema akaunti hiyo ilifunguliwa Benki kuu mwaka 2004 na hadi jana, akaunti ile ilishafikia dola milioni 122 za Marekani,” alisema Kafulila.
Alisema kuwa fedha hizo ziliwekwa kwa lengo maalumu kutokana na mgogoro uliokuwepo kati ya IPTL na Tanesco ili ziweze kusaidia malipo baada ya mgogoro kuisha katika Baraza la Usuluhishi wa Kibiashara la ISCID.
Alifafanua kuwa IPTL ilikuwa ni makubaliano ya kufanya kazi kwa kampuni mbili ambazo ni VIP Engineering ya Tanzania iliyokuwa na hisa asilimia 30 na Mecmer ya Malaysia ambayo ilikuwa na asilimia 70 ya hisa.
Kafulila alisema kuwa anao ushahidi kuwa PAP ilikuwa imenunua hisa za VIP tu na kwamba hakukuwa na vielelezo vya kununua Mecmer kwa kuwa kampuni hiyo tayari ilishapoteza uhalali wake kwa kuwa ilikuwa chini ya muflisi nchini Malaysia.


EmoticonEmoticon