UKWELI KUHUSU ESCROW ACCOUNT WAWEKWA HADHARANI

Taarifa zaidi kuhusu akaunti ya Escrow

TAARIFA zaidi zimezidi kupatikana kuhusu sakata la Escrow, linalohusisha makubaliano baina ya serikali, Kampuni ya kufua umeme ya Independet Power Tanzania Limited (IPTL) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama wakala wa Escrow kuwa yalikuwa ni makubaliano ya kisheria.

Makubaliano hayo yalilenga kumaliza mgogoro wa kimaslahi baina ya wabia, ambao ni Kampuni ya VIP na Mechmar kutoka nchini Malaysia, ambapo VIP ilikuwa inamlalamikia mbia mwenzake kuhusu thamani ya hisa zake.

Hali hiyo ilisababishwa na mkataba wao, ambao ulikuwa ikimtaka kampuni ya VIP kufanya kazi za utekelezaji ikiwemo misamaha ya kodi, ofisi itakayofungwa mtambo huo wa uzalishaji umeme megawati 100, ambapo mtambo huo ulifungwa Tegeta.

Taarifa zaidi kuhusu mkataba huo, ilieleza kazi zitazofanywa na Kampuni ya VIP ni asilimia 30 ya
hisa zote huku Mechmar ikibaki na hisa ya asilimia 70 kutokana na kutoa mtaji wa uzalishaji umeme.

Kutokana na hali hiyo, VIP haikuwa tayari kuanzisha mgogoro wa kimaslahi baina yake na Mechmar, wakati kesi yao ikiendelea Mahakama Kuu ndipo VIP ikatoa pendekezo la kuzuia kulipwa kwa IPTL hadi mgogoro wao utakapoisha.

Pendekezo liliungwa mkono na serikali, ambaye ni mnunuzi wa umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), na kutengeneza makubaliano kisheria ya pamoja yaliyoitwa ‘Escrow Agreement’ yaliyosainiwa na pande zote tatu ikiwemo serikali, IPTL na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ilikuwa kama wakala wa Escrow Julai 5, 2006.

Ilisema makubaliano hayo ya kisheria ilipelekea kufunguliwa kwa akaunti maalumu ya pamoja baina ya serikali, IPTL na BoT ili kutunza fedha zote za malipo ambazo IPTL walipaswa kulipwa kutokana na mauzo ya umeme waliokuwa wakiyafanya Tanesco kipindi chote cha mgogoro.

Katika makubaliano hayo, serikali iliingia kama mnunuzi wa umeme kupitia Tanesco na ilikuwa na wajibu wa kupeleka fedha katika akaunti ya Escrow badala ya kuwalipa IPTL moja kwa moja kama ilivyokuwa awali.

Ilieleza zaidi BoT wao walikuwa wakala wa Escrow na kazi yao ni kupokea, kutunza fedha na kutoa taarifa kwa pande zote zilizosaini makubaliano hayo huku IPTL yenyewe ikiwa ndio wazalishaji wa umeme.

Makubaliano hayo yalieleza kwamba, pindi mgogoro utakapoisha BoT itapaswa kutoa fedha hizo kwa IPTL ndani siku 60, baada ya pande zote kuafikiana.

Akizungumzia kuhusu Escrow, Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria wa IPTL/PAP, Joseph Makandege alisema wapo mbioni kuweka kila kitu katika wazi ili Watanzania wapate ukweli kuhusu Escrow.

Alisema Escrow lilikuwa jambo la kisheria baina ya wabia na serikali kama mpokea huduma, ambalo walilimaliza wao wenyewe kwa makubaliano yao ya kisheria.

“Hakuna kitu chochote ovu hapa, mengi yanayozungumzwa katika mitandao ni ya zamani na si mapya, ambayo yamemalizika kisheria,’’ alisema.

Hivyo, alisema IPTL/PAP ni kampuni makini isiyokuwa na chembe ya kifisadi na imefika hapo baada ya kupita hatua zote za kisheria, ikiwemo kununua hisa za VIP na Mechmar.

Alisema wanazidi kuwaomba watanzania, wawaamini na kuendelea kuwaamini kwa kuwa hakuna vitendo vya ufisadi.

source Habari Leo


EmoticonEmoticon