Waziri auawa Korea Kaskazini kwa madai ya kusinzia katika mkutano

Serikali ya Korea Kusini imesema waziri wa elimu nchini Korea Kaskazini ameuawa na maafisa wa serikali.
Tangazo la kifo cha Kim Yong-jin limetolewa na wizara ya muungano ya Seoul na limetolewa siku chache baada ya taarifa za gazeti moja kusema maafisa wawili wakuu wa Korea Kaskazini waliuawa kwa kulipuliwa kwa makombora ya kutungua ndege.
Gazeti hilo lilisema wawili hao waliuawa mapema mwezi huu.
Waziri huyo wa elimu anadaiwa kuchunguzwa kwa madai ya kuhusika katika ufisadi baada yake kusinzia katika mkutano wa kiongozi wan chi hiyo Kim Jong-un.
SOURCE: BBC SWAHILI

Stesheni "zilizomtusi" Magufuli zafungiwa


Serikali ya Tanzania imezisimamisha kwa muda stesheni mbili za redio ,radio 5 na Magic FM kwa madai ya kumtusi rais Magufuli na kuchochea ghasia nchini.
Mapema mwezi huu ,serikali pia ilipiga marufuku gazeti moja kwa kuchapisha 'habari za uongo'.
Waziri wa mawasiliano Nape Nnauye amesema ameagiza kamati ya maadili kuzichunguza idhaa hizo na kupendekeza hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yake.
Marufuku ya steheni hizo mbili inajiri huku hali ya wasiwasi ikitanda nchini humo kufuatia hatua ya upinzani kufanya mikutano yake nchi nzima.
Kulingana na muungano wa upinzani nchini humo CHADEMA,mikutano hiyo kwa jina UKUTA ,inalenga kupinga kuidhinishwa kwa sheria ya uhalifu wa mitandaoni inayokandamiza uhuru wa kujieleza ,kufutwa kazi kwa wafanyikazi wa serikali kiholela pamoja na marufuku ya mikutano ya kisiasa ya upinzani.
Ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam umetoa ushauri wa kusafiri kwa raia wake ukiwaonya kutozuru maeneo ambayo mikutano hiyo itafanyika.
Habari:BBC SWAHILI

Maurinho Rasmi Manchester United


 picha: Maurinho na Van Gaal.




Imeshafahamika rasmi sasa kuwa kocha Jose Maurinho atachaguliwa na Uongozi wa Manchester United "Red Devils" kuwa Manager Mpya wa timu hiyo na kuziba Pengo la Van Gaal ambaye anaachia mikoba kilabuni hapo.

Joaquin "El Chapo" Guzman kuhamishiwa Marekani


Mexico imeidhinisha kuhamishiwa Marekani mlangunzi mkuu wa madawa ya kulevya, Joaquin Guzman, almaarufu El Chapo, ili ashtakiwe kwa mauaji na ulanguzi wa madawa ya kulevya.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya imesema kuwa Marekani imehakikishia taifa hilo jirani kuwa Guzman hatahukumiwa kifo katika kesi zinazomkabili.

SOURCE:BBC SWAHILI

CUF: HATUMTAMBUI SHEIN KAMA RAIS



Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar kimesema hakimtambui Dkt Mohamed Ali Shein aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi uliopita.
Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), wakizungumza kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi huo ambao chama hicho kilisusia, wamesema hawamtambui Dkt Shein kama rais wa visiwa hivyo.
“Tangu mapema, tangu Jecha (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha) alipofuta uchaguzi, tulisema waziwazi kwamba haikuwa halalali. Walipoitisha uchaguzi wa marudio, tulisema waziwazi uchaguzi huo sisi hatuutambui na tukawataka wananchi wasipige kura,” amesema Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.
Bw Hamad alikuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana na ambao matokeo yake yalifutwa na tume.
“Kama Rais ametokana na mchakato ambao hamkuutambua nyinyi tangu mwanzo, sasa leo kuja kusema hatumtambui kwa nini iwe ni haramu? Hatumtambui.”
Chama hicho kimesema kitatumia njia za kidemkrasia kulalamika dhidi ya Dkt Shein na serikali yake.
Aidha, kimeiomba jamii ya kimataifa kuwawekea vikwazo watu binafsi waliofanikisha uchaguzi huo wa marudio ambao chama hicho kimesema ulikuwa “uongozi haramu”.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama Twaha Taslima amesema chama hicho hakiko tayari kuwa sehemu ya serikali mpya.
"CUF haitoshirikiana na serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na katiba ya Zanzibar, kinyume na sheria ya uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu," amesema.
Wiki iliyopita, Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani (MCC) lilisitisha ufadhili wa $472milioni kwa Tanzania likilalamikia uchaguzi visiwani Zanzibar na utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.
Pesa hizo zilikuwa za kutumiwa katika miradi ya kusambaza umeme.
CUF imesema upo uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo ka ikiwa uchaguzi huo utarudiwa basi usimamiwe na ujumbe wa kimataifa kwani wasimamizi wa ndani wamepoteza uhalali
Chama tawala visiwani humo kimebeza tamko hilo la CUF ana kusema kuwa Wazanzibari ni watu makini na kwamba hawawezi kumnyima ushirikiano Rais wao ambaye anafanya kazi kuwaletea maendeleo
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ameiambia BBC kwamba Rais Shein anao pia uwezo wa kutengeneza serikali hata bila ushiriki wa chama cha CUF
"CUF wanafanya upotoshaji. Katiba haijamfunga Rais kukamilisha utengenezaji wa serikali yake. Na hivi tunapozungumza, muda si mrefu atakamilisha serikali yake na atajumuisha Wazanzibari na kufanya nao kazi" alisema Vuai.
Hii ni mara ya kwanza kwa Chama cha CUF kutoa tamko tangu kurudiwa kwa uchaguzi ambao waliususia.
SOURCE: BBC SWAHILI

Mwanaume aliyeota mizizi



Serikali ya Bangladesh imesema itagharimia upasuaji wa kumtibu mwanamume ambaye anaugua ugonjwa unaofanya mtu kupata dutu zinazofanana na mizizi ya mti mwilini.
Waziri wa afya wa Bangladesh Mohammad Nasim alitangaza hilo baada ya kumtembelea Abul Bajandar, hospitalini Alhamisi.
Bw Bajandar anaugua ugonjwa ambao kisayansi unajulikana kama epidermodysplasia verruciformi.
Ni ugonjwa wa kinasaba ambao humfanya mtu kuota vidutu kwenye ngozi. Hujulikana sana kama “ugonjwa wa binadamu mti”.
Alianza kuota vidutu miaka 10 iliyopita.
“Awali, nilidhani hazina madhara,” Bw Bajandar ameambia AFP
"Sasa zimeongezeka na nyingine zina urefu wa inchi mbili hadi tatu katika mikono yangu miwili. Kuna nyingine miguuni,” amesema.
Bw Bajandar alisafiri India kutafuta matibabu lakini familia yake haingemudu gharama.
Sampuli za damu yake na ngozi zitapelekwa kwenye maabara moja Marekani kuchunguzwa zaidi, profesa Abdul Kalam, ambaye ni mtaalamu wa upasuaji wa ngozi ameambia BBC.
Atatibiwa nchini Bangladesh baada ya matokeo ya uchunguzi kutolewa.
Bw Bajandar ni mmoja wa watu watatu wanaougua “ugonjwa wa binadamu mti” duniani, mkurugenzi wa hospitali ya chuo cha Dhaka, Samanta Lal Sen ameambia AFP.
Ni mara ya kwanza kwetu kupata kisa kama hicho hapa Bangladesh.
source: BBC Swahili

BASTOLA YA DHAHABU YA GADDAFI IKO WAPI?

Miaka minne iliyopita, waasi nchini Libya walisherehekea kifo cha aliyekuwa rais Muammar Gaddafi.
Bastola yake iliyofunikwa imepambwa kwa dhahabu iliinuliwa juu na wapiganaji hao, ikiwa ishara ya ushindi dhidi ya utawala wa Gaddafi.
Kwa furaha, wapiganaji hao waliipokezana kwa zamu!
Bastola hiyo ilikuwa silaha binafsi ya Gaddafi, japo kwa wakati huo ilibadilika na kuwa ishara ya ushindi kwa waasi, na uhamisho wa mamlaka, katika mwamko mpya wa Libya.
Mjini Misrata, kilomita 200 mashariki mwa mji mkuu wa Tripoli, ndipo inapoaminika kuwa bunduki hiyo ipo kwa sasa.
Mwandishi wa BBC Gabriel Gatehouse alishuhudia sherehe hizo zilizohusisha bastola hiyo moja kwa moja.
Na baada ya miaka minne, Gabriel Gatehouse, amerejea Libya kutafuta bastola hiyo na pia kuona jinsi maisha yalivyo kwa waasi waliomwangamiza Gaddafi.
Anaanza kwa kumtembelea mdokezi wake wa zamani Anwar Suwan.
Alihusika sana katika mapinduzi Misrata. Gaddafi alipouawa, wapiganaji walipeleka mwili wake kwa Anwar, na Anwar akauweka mwili huo hadharani watu wauone, ukiwa umewekwa kwenye jokofu kubwa la kuhifadhia nyama.
Anapomwambia kwamba anamtafuta mtu aliye na bunduki ya Gaddafi, mara moja anamfikiria Omran Shabaan, mmoja wa wapiganaji waliomkamata Gaddafi.
Kwenye kanda ya video iliyopigwa na waasi kwa kutumia simu, Shabaan anasikika akiwasihi watu wasimuue Gaddafi.
Mwingine aliyekuwepo siku hiyo, Ayman Almani, anamwonyesha Gatehouse video aliyoichukua siku hiyo, ambayo haijawahi kuonyeshwa kwenye vyombo vya habari awali.
Inaonyesha nyakati za mwisho za kiongozi huyo wa kiimla, anaonekana akitokwa na damu na kuwasihi watu wasimuue.
Omran Shabaan aligeuka na kuwa shujaa. Alipigwa picha akiwa na video hiyo iliyopambwa kwa dhahabu na akawa ishara ya matumaini kwamba Libya ingejikwamua.
Lakini hili halikuwa na mapigano yameendelea.
Mwaka 2012, Shabaan mwenyewe alikamatwa na wafuasi wa Gaddafi eneo la Bani Walid. Walimpiga na kumtesa. Wapiganaji wa Misrata walipofanikiwa kumkomboa, walikuwa wamechelewa sana. Alifariki kutokana na majeraha akitibiwa hospitali moja Ufaransa.
Anwar Suwan anamwambia Gatehouse kwamba huenda Shabaan alikuwa na bastola hiyo alipokamatwa na wafuasi wa Gaddafi.
Huenda imo mikononi mwa wafuasi hao wa Gaddafi.
Kwenye simu yake ya rununu, Gatehouse ana picha aliyoipiga tarehe 20 Oktoba mwaka 2011 siku ambayo Gaddafi aliuawa.
Ninamuonyesha picha hiyo. Ni picha ya kijana mmoja, akiwa amevalia shati la rangi ya samawati, na kofia ambayo ni maarufu na wachezaji wa mpira wa magongo wa New York Yankees.
“Mohammed Elbibi,” mtu mmoja anamtambua.
Kwenye picha, Mohammed anaonekana akitabasamu huku akibebwa juu kwa juu na wenzake, akiwa ameinua bastola hiyo.
Anwar anasema hajui yaliyomsibu Mohammed lakini anaahidi kusaidia kumtafuta.
Baada ya muda mrefu, Gabriel Gatehouse, alipata anwani yake Mohammed Elbibi, kijana aliyekuwa kwenye picha aliyoipiga akiwa ameinua bastola hiyo.
Alimpigia simu na akakubali kukutana naye.
Anapomwonyesha picha yake, anatabasamu na kusema, "naikumbuka, nilikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo".
"Bunduki unayo?" Gabriel anauliza.
Mohammed angali anaihifadhi bastola hiyo!
Ni bastola ya milimita 9 aina ya Browning, iliyofunikwa kwa safu nyembamba ya dhahabu ikiwa imepambwa kwa miundo ya maua.
Mohammed anasema kamwe hakumuua Gaddafi.
Anasema aliokota bunduki hiyo karibu na mahali ambapo Gaddafi alikamatwa, na katika mtafaruku uliokuwepo, na pia alipoonekana na bastola hiyo, waasi wengine walidhani Mohammed ndiye aliyemuua Gaddafi, na papo hapo akakuwa shujaa wa mapinduzi nchini Libya!
Hata hivyo Mohammed anaishi kwa woga.
Wafuasi wa Gaddafi wanatishia maisha yake.
"Tafadhali elezea ulimwengu kuwa sio mimi niliyemuua Gaddafi," Mohammed anasema.

SOURCE: BBC SWAHILI

MILIPUKO YATOKEA BURUNDI


Watu kadhaa wameripotiwa kujeruhiwa vibaya katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura kufuatia milipuko 3 ya guruneti.
Duru zinasema kuwa takriban watu wanne wamejeruhiwa baada ya watu wasiojulikana kutupa gruneti nje ya jumba la posta mjini Bujumbura.
Mlipuko mwengine ulitokea nje ya afisi za kampuni inayotoa huduma za simu nchini humo Lumitel.
Mlipuko wa tatu ulisikika takriban nusu saa baadaye katika soko la zamani.
Hadi tulipochapisha taarifa hii hakuna maelezo kamili hayajatolewa kuhusu nani aliyetekeleza mashambulizi hayo na kwanini.
Machafuko nchini humo yalitibuka mwezi Aprili mwaka wa 2015 baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania uchaguzi katika muhula wake wa tatu.
Wapinzani wake walisema Nkurunziza alikuwa anakiuka katiba ya taifa na kisha maandamano yakaanza kukotokea.
Kulitokea jaribio la mapinduzi ambayo ilizimwa na kisha rais huyo akaibuka mshindi katika uchaguzi ambao ulisusiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa upinzani.
Mwandishi wa BBC aliyeko huko Prime Ndikumagenge, anasema kuwa mashambulizi haya leo ni ya kipekee kwa sababu ni mara ya kwanza kuwahi kutokea mchana.
''kumekuwa na mashambulizi mengi nchini ,lakini hii ndio mara ya kwanza kwa mashambulizi ya aina hii kutokea mchana''.
Takriban watu 439 wameuawa huku wengine 240,000 wakitoroka nchini kuwa wakimbizi nje ya nchi kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Mwezi uliopita shirika linalopigania haki za kibinadamu Amnesty International walisema kuwa picha za setlaiti zinaonesha uwezekano wa kuweko kwa makaburi 5 ya halaiki nje ya Bujumbura.
Maafisa wa usalama wanalaumiwa kwa kuua watu mwezi desemba mwaka uliopita.
SOURCE: BBC SWAHILI
MAGUFULI ASIMAMISHA KAZI NA KURUDISHA MABALOZI NCHINI

MAGUFULI ASIMAMISHA KAZI NA KURUDISHA MABALOZI NCHINI

1. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

1.1 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.

1.2 Aidha, baada ya utenguzi huo, Bwana Dickson E. MAIMU amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, pamoja na wafuatao:

1.2.1 Bwana Joseph MAKANI, Mkurugenzi wa TEHAMA
1.2.2. Bi Rahel MAPANDE, Afisa Ugavi Mkuu
1.2.3 Bi Sabrina NYONI, Mkurugenzi wa Sheria
1.2.4 Bwana George NTALIMA, Afisa usafirishaji

1.3 Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

1.4 Hivyo, Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.

1.5 Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.

1.6 Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.

2.0 Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

2.1 Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.

2.2 Rais ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha. Leo hii Mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au Mwandamizi aliye chini yao. Mabalozi hao ni:

2.2.1 Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan

2. 2.2 Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia.

2.3 Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan KALLAGHE. Anarejea Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa atakapopangiwa kazi nyingine.

2.4 Kwa maana hiyo, vituo vya Ubalozi vifuatavyo viko wazi:

2.4.1 London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. KALLAGHE

2.4.2 Brussels, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous KAMALA kuchaguliwa kuwa Mbunge.

2.4.3 Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dkt. James Alex MSEKELA.

2.4.4 Tokyo, Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Bibi Batilda BURIANI

2.4.5 Kuala Lumpar, Malaysia, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Aziz Ponray MLIMA, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.

2.4.6 Brasilia, Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Bwana Francis MALAMBUGI.

3.0 Tawala za Mikoa

3.1 Rais ametengua uteuzi wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.

3.2 Nachukua nafasi hii kuwahimiza viongozi wote katika Utumishi wa Umma, na watumishi wote wa umma, kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu wao.

3.3 Napenda kusisitiza kuwa Rais na sisi tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine. Tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua. Mambo yafuatayo ni muhimu:

4.0 Utumishi wa Umma

4.2.1 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi.

4.2.2 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu asipate kigugumizi kuchukua

hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.

4.2.3 Lazima uongozi na watumishi wa umma wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima. Kwa sababu hiyo:

a) Kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

b) Kwenye kila Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati. Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu. Ikibidi wananchi wafike Ikulu ina maana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.

c) Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.

d) Kila ofisi ya Serikali iwe na utaratibu wa kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo, na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
25 Januari, 2016
 
SIGNATURE

Ada ya Whatsapp Yafutwa



Wamiliki wa app ya mawasiliano ya WhatsApp wamefuta ada ambayo watumizi wake wamekuwa wakitakiwa kulipa kila baada ya mwaka mmoja.
Wamiliki wa huduma hiyo wamekuwa wakiwatoza watu $0.99 kila mwaka baada ya kuitumia kwa mwaka mmoja.
Ada hiyo ilianza kutozwa miaka michache iliyopita lakini kampuni hiyo inasema haijakuwa na manufaa sana.
Taarifa kutoka kwa wamiliki wa WhatsApp inasema: “Watu wengi wanaotumia WhatsApp hawana kadi za benki na wengine huwa na wasiwasi kwamba baada ya mwaka mmoja watazuiwa kuungana tena na marafiki na jamaa.”
“Kwa hivyo, wiki chache zijazo, tutaondoa ada zote tunazotoza wa wanaotumia aina mbalimbali za app yetu na hutatozwa tena pesa ili kutumia WhatsApp.”
Kwa sasa, WhatsApp, ambayo humilikiwa na Facebook, hutumiwa na watu bilioni moja na kampuni hiyo inatumai kuondolewa kwa ada kutavutia watu wengi zaidi.
SOURCE: BBC SWAHILI
PICHA: BBC SWAHILI

Mwanamume mmoja nchini Kenya ameshtakiwa kusambaza picha alizodai ni za wanajeshi wa Kenya waliouawa nchini Somalia akitumia WhatsApp.


Eddy Reuben Illah ameshtakiwa kwa kueneza: “Picha zinazodaiwa kuwa za miili ya maafisa wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF), waliodaiwa kushambuliwa na kuuawa eneo la El-Adde nchini Somalia ukijua kwamba ni za uchochezi na zingesababisha hofu na wasiwasi miongoni mwa raia.”
Anadaiwa kusambaza picha hizo kwenye kundi la watumiaji wa WhatsApp kwa jina A young peoples union (Muungano wa vijana).
Bw Illah amekanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mwandamizi wa Kiambu, mji ulio karibu na Nairobi, Bw Justus Mutuku.
Juhudi za wakili wake Bw Edwin Sifuna kutaka aachiliwe huru kwa dhamana huru zimegonga mwamba na akatakiwa kuweka dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa Sh50,000, gazeti la Daily Nation limeripoti.
Kesi hiyo itatajwa Februari 2 na kuanza kusikilizwa Februari 12.
SOURCE: BBC SWAHILI
PICHA: BBC SWAHILI

Bulaya Amtaka Wasira Mahakamani




By Jesse Mikofu, Mwananchi
Mwanza. Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya amemtaka aliyekuwa mpinzani wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Stephen Wasira (CCM) kuacha kujificha nyuma ya wapigakura, badala yake ajitokeze kortini kupinga ushindi wake.
Kupitia kwa wakili wake, Tundu Lissu, mbunge huyo alidai mbele ya Jaji Ramadhan Mohamed wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuwa, ingawa jina la Wasira halimo kwenye orodha ya wadai, lakini ametajwa kwenye hoja zote za walalamikaji ambao pia wamekiri kwa hati ya kiapo kuwa hoja walizowasilisha mahakamani walizipata kutoka kwake.
Bulaya alikuwa akiwasilisha hoja za pingamizi aliloweka dhidi ya shauri la madai namba moja la mwaka 2015 lililofunguliwa mahakamani hapo na Magambo Masato na wenzake watatu wakiiomba mahakama kutengua matokeo yaliyompa ushindi mbunge huyo aliyekuwa kada wa CCM kabla ya kuhamia Chadema.
“Kwa nini Wasira asijitokeze mwenyewe kuja mahakamani kudai haki yake iliyokiukwa badala ya kujificha nyuma ya wapigakura ambao kimsingi walipata haki yao ya kikatiba ya kupiga kura?” alihoji Lissu.
Wakili huyo alidai maelezo yote kwenye hati ya madai ya walalamikaji hayataji haki yoyote ya mpigakura iliyokiukwa, bali anayedaiwa kunyimwa haki ni Wasira ambaye siyo mmoja wa walalamikaji.
Bulaya anaiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi hayo akidai walalamikaji hawana haki kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi.
Miongoni mwa madai ya msingi ya walalamikaji wanaowakilishwa na mawakili Constantine Mutalemwa na Denis Kahangwa, wanadai Wasira alikataliwa ombi la kuhesabu wala kuhakiki kura.
Walalamikiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bunda Mjini. Uamuzi wa pingamizi hilo utatolewa Januari 25.

SOURCE: GAZETI LA MWANANCHI
PICHA: MWANANCHI 

Masauni aitaka Nida iharakishe vitambulisho




By Bakari Kiango
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni amesema hajaridhishwa na kasi ya usajili wa watu kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa na kuagiza ziongezwe juhudi kutekeleza suala hilo.
Masauni alitoa kauli hiyo jana, alipofanya ziara ya kutembelea makao makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na kuangalia sehemu ya uhakiki, uingizaji wa taarifa na uandaaji wa vitambulisho.
Alisema licha ya Nida kutimiza agizo la Waziri wa wizara hiyo, Charles Kitwanga aliyeitaka kupanga mkakati wa namna itakavyowasajili watu waliofikia umri wa miaka 18, lakini kasi bado ni ndogo kusajili watu ni tofauti ilivyoanza hadi hivi sasa.
“Suala hili limetimiza miaka mitatu. Lakini hadi sasa wamefikia watu milioni sita, idadi hii ni ndogo nahitaji iongezeke zaidi,” alisema Masauni.
Aliitaka Nida kuharakisha usajili wa watu ili kwenda sambamba na agizo la Kitwanga aliyeitaka NIDA kuandikisha watu wasiopungua milioni 15 katika kipindi cha miezi sita.
“Najua mazungumzo yanaendelea vizuri kati yenu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mkipata vifaa 5,000 vitawasaidia kwenye suala hili,” alisema Masauni.
Pia, alitao rai kwa wananchi kutotengeneza vitambulisho nje ya utaratibu uliopangwa na Serikali na kwamba, atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu alisema wakati wanaanza usajili walikuwa na vifaa 226 na kila kimoja kilikuwa kinaandikisha watu 50 kwa siku, hali iliyowawia vigumu kuandikisha watu wengi kwa wakati.
Hata hivyo, Maimu alisema mwezi huu wanatarajia kupokea mashine 5,000 za BVR kutoka NEC ambazo wana imani zitakuwa msaada mkubwa kuharakisha uandikishaji wa vitambulisho.


“Sasa hivi tumeambiwa mashine hizi zipo katika matengenezo baada ya uchaguzi kwisha na yakikamilika tutapewa,” alisema.

SOURCE: Gazeti la Mwananchi Tarehe 16 January,2016.
PICHA: GAZETI LA MWANANCHI

Kategori

Kategori