MILIPUKO YATOKEA BURUNDI


Watu kadhaa wameripotiwa kujeruhiwa vibaya katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura kufuatia milipuko 3 ya guruneti.
Duru zinasema kuwa takriban watu wanne wamejeruhiwa baada ya watu wasiojulikana kutupa gruneti nje ya jumba la posta mjini Bujumbura.
Mlipuko mwengine ulitokea nje ya afisi za kampuni inayotoa huduma za simu nchini humo Lumitel.
Mlipuko wa tatu ulisikika takriban nusu saa baadaye katika soko la zamani.
Hadi tulipochapisha taarifa hii hakuna maelezo kamili hayajatolewa kuhusu nani aliyetekeleza mashambulizi hayo na kwanini.
Machafuko nchini humo yalitibuka mwezi Aprili mwaka wa 2015 baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania uchaguzi katika muhula wake wa tatu.
Wapinzani wake walisema Nkurunziza alikuwa anakiuka katiba ya taifa na kisha maandamano yakaanza kukotokea.
Kulitokea jaribio la mapinduzi ambayo ilizimwa na kisha rais huyo akaibuka mshindi katika uchaguzi ambao ulisusiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa upinzani.
Mwandishi wa BBC aliyeko huko Prime Ndikumagenge, anasema kuwa mashambulizi haya leo ni ya kipekee kwa sababu ni mara ya kwanza kuwahi kutokea mchana.
''kumekuwa na mashambulizi mengi nchini ,lakini hii ndio mara ya kwanza kwa mashambulizi ya aina hii kutokea mchana''.
Takriban watu 439 wameuawa huku wengine 240,000 wakitoroka nchini kuwa wakimbizi nje ya nchi kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Mwezi uliopita shirika linalopigania haki za kibinadamu Amnesty International walisema kuwa picha za setlaiti zinaonesha uwezekano wa kuweko kwa makaburi 5 ya halaiki nje ya Bujumbura.
Maafisa wa usalama wanalaumiwa kwa kuua watu mwezi desemba mwaka uliopita.
SOURCE: BBC SWAHILI


EmoticonEmoticon