IPTL YANG'AA,MAHAKAMA KUU YAAMURU ISIBUGHUZIWE









MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imeiamuru Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong  (SCBHK) na Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (Tanesco) kuacha kuingilia utulivu, umiliki, usimamizi na utawala wa mitambo ya ufuaji umeme ya Harbinder Singh Sethi iliyopo Tegeta, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi ya msingi.
Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions Limited (PAP) zilifungua kesi kwa kuhoji uhalali wa maamuzi ya Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) dhidi ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) na Martha Renju (anayedaiwa kuwa msimamizi wa mali zake), iliyotolewa katika kesi ya ICSD namba ARB / 10/20.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Dk. Fauz Twaib na kusomwa kwa niaba yake na Jaji Amri Msumi Hamisi, Jaji Twaib aliamuru Tanesco kutofanya biashara yoyote na SCB-HK au Martha Renju kwa niaba ya IPTL / PAP bila ya idhini ya kimaandishi kutoka IPTL / PAP.
“Wadaiwa kwa pamoja wanazuiliwa kufanya utekelezaji wa maamuzi iliyotolewa katika chombo cha kimataifa ya ICSD yenye namba ARB / 10/20 na kusambazwa kwa wahusika Februari 12, 2014, kwa namna yoyote ile, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya mdai, ” ilisomeka sehemu ya hukumu hiyo.
Tanesco pia imezuiwa kutolipa kwa SCB-HK na Martha Renju malipo yoyote wanayostahili IPTL / PAP bila ya idhini ya maandishi kutoka kwa IPTL / PAP.
Mahakama pia imeizuia Tanesco kutotekeleza au kukubaliana na au kuyatekeleza maamuzi ya ICSID, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi.
Pia mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja ya mwanasheria wa SCB-HK, Charles Morrison, ambaye alisema Mahakama Kuu ya Tanzania haipaswi kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya ombi hilo sababu Tanzania ni mwanachama wa ICSID ambayo pia inajulikana kama Washington Convention au ICSID .
Kwa mujibu wa Jaji Twaib, Wakili Morrison alionya kuwa kama Tanzania haitotii wajibu huo, itajiweka sehemu mbaya katika nyanja ya kimataifa.
SOURCE:TANZANIA DAIMA 02,OCTOBER,2014


EmoticonEmoticon