Kilaini: Sitta ana msongo wa mawazo




Dodoma. Sasa ni wazi kwamba Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta ameingia katika mgogoro na viongozi wa dini.
Wakati jana Sitta akirejea kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kwamba waraka uliotolewa na viongozi wa Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu mchakato wa Katiba kwamba “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”, viongozi hao wamesema mwanasiasa huyo ahurumiwe kwa kuwa “ana msongo wa mawazo”.
Kauli ya Sitta
Sitta alisema nia ya baadhi ya viongozi hao wa dini ni kuliingiza Taifa katika machafuko, jambo ambalo alisema kama mtu mzima na mzee, hatalivumilia.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
Sitta alilieleza Bunge hilo kuwa lugha iliyotumika kuandika waraka huo aliokuwa nao na kusoma baadhi ya vipengele vyake, haina staha na haifai hata kidogo kutolewa na watu ambao wanahubiri dini na amani.
“Moja ya vitu ambavyo watu wanatakiwa kuviona, hivi wanaposema kuwa rais asimamishe mchakato wa Katiba, wanakuwa na maana gani? Hivi ni Ukristo huo kweli unaotokana na utukufu wa Mungu?” alihoji Sitta huku akishangiliwa na wajumbe. Alikwenda mbali akiifananisha lugha iliyotumika kuandaa waraka huo na ile aliyozoea kuisikia kutoka kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akinukuu sehemu ya waraka huo iliyosema “mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba afanye kazi bila ya ubabe,” alisema huo ni uongo kwani anafanya kazi kwa weledi mkubwa.
“Jamani, mimi ni Mkristo na wala sina ubabe wala kiburi. Hivi hawa wanaotutukana kule nje hawawaoni? maneno mangapi yanasemwa juu yetu na watu wale, hivi hii siyo siasa jamani? Waraka huo wa maaskofu umesomwa kila mahali na makanisani, unawezaje kusema Rais aifufue Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati tayari tume hiyo ilishajifufua yenyewe kwa kujibizana na Bunge kila wakati?”
Sitta aliendelea kueleza kuwa akiwa mzee na mtu mzima, atasimamia jambo hilo na kuona nchi inakaa katika hali ya utulivu kwa kuwa nchi haina dini na itaendelea kuwa hivyo wakati wote.
Aliwatuhumu maaskofu hao kukusanywa jijini Dar es Salaam na kundi la Ukawa ili kutoa waraka huo, kisha kubariki usomwe makanisani wakati hawajui kuwa ndani ya makanisa kuna makundi mbalimbali ya waumini, ambao baadhi yao ni wana-CCM.
Bila ya kumtaja, alimtuhumu mmoja wa maaskofu hao kuwa ameapa kwamba atawaelimisha wafuasi wake ili siku za usoni viongozi kama Sitta washughulikiwe, lakini akasema anamtaka aendelee na mpango wake huo kwa kuwa haogopi na kwamba kazi ya askofu si kuwatisha wanasiasa.
“Kama kazi ya uaskofu ni kuwatisha wanasiasa basi, aendelee maana ah, labda Kanisa limebadilika siku hizi.”
Majibu ya maaskofu
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema kauli ya Sitta inaonyesha kuwa amechoshwa na mwenendo wa Bunge la Katiba. “Sikutarajia kiongozi kama huyo kutoa kauli mbaya kama hiyo kwa Taifa zima. Sikutegemea mheshimiwa kama huyo kusema maneno kama hayo… huenda ana stress (msongo wa mawazo). Hata ikiwa hivyo, hakupaswa kutoa kauli nzito kama hiyo. Anatakiwa kufahamu kuwa waraka huo umetoka kwa Wakristo wote hapa nchini,” alisema Askofu Kilaini.
“Hata kama anakinzana na yale yaliyoandikwa kwenye huo waraka, nadhani kuna namna ya kistaarabu ya kupingana nao. Aseme, siyo kudharau mawazo ya wengine. Kama anadharauliwa basi asifanye hivyo kwa wengine.”
Makamu wa rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alisema Sitta atahukumiwa na historia ya Tanzania kutokana na kauli hiyo aliyoiita ya kejeli na kupuuza maoni ya Watanzania.
Niwemugizi, ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, alisema, “Nimesikitishwa sana na kauli zake, nilijua ni mstaarabu, msikivu wa kuzingatia ushauri, kwa hiyo nikamheshimu sana katika uongozi wake, lakini kumbe amepungukiwa na busara. Historia lazima itamhukumu tu siku zijazo.”
Alisema kauli ya Sitta pia inaonyesha “jinsi gani tulivyo na matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wetu. Madaraka yanawafanya kuwa na kiburi na dharau, lakini hatushangai sana kwa sababu ya msingi wa chama chake.”
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), lililopo Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema: “Sitta alijijengea heshima kubwa sana kwa Watanzania, hafanani na fikra ya kuzungumza kauli hizo. Nashangaa kwa nini ameamua kujitoa kafara. Hata kama kuna jambo limekosewa, siyo sahihi kwake kutoa kauli kama hizo. Kazi ya miezi mitatu inampotezea heshima yake ya miaka 30 kwenye uongozi wake. Inasikitisha sana.”
na lazima itamgharimu kwa sababu hana nafasi tena ya kusahihisha makosa.”
source Mwananchi


EmoticonEmoticon