MKUTANO WA KIKWETE NA UKAWA NI KISHINDO




Zanzibar/Dar/Dodoma/Arusha. Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kutaka kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge kupitia muungano wao wa Kituo cha Demokrasia (TCD), umeibua mjadala katika sehemu mbalimbali nchini huku wasomi na wanasiasa wakitoa angalizo.
Miongoni mwa watu walihojiwa, pamoja na kukubaliana na uamuzi huo wa kutafuta mwafaka, suala la Bunge kuendelea na vikao kabla ya maridhiano hayo limeendelea kuiweka Katiba Mpya njiapanda.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Kibodya amesema, “Tusiogope kuingia gharama kuanza upya mchakato wa kupata Katiba Mpya iwapo hakutapatikana maridhiano. Tunatakiwa kujifunza kuanzia hapo.”
Kibodya alisema ni ngumu kwa Ukawa kuridhia mambo yatakayopigiwa kura kwa sababu mengi waliyapinga na ndiyo ilikuwa sababu ya umoja huo kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu.
“Katiba ni ya nchi, si mali ya vyama vya siasa, hivyo maridhiano ni muhimu. Kikubwa wakati wa utungaji wa Katiba ni lazima yawepo maridhiano ya kisiasa. Rais Kikwete anatakiwa kutumia hekima katika mkutano huo na washiriki wote kwa ujumla waondoe vichwani mwao kwamba sisi ‘tumeshinda na wao wameshindwa’.
Alisema pamoja na mambo mengine, ni bora mchakato wa kuandika Katiba Mpya ukachukua muda mrefu na gharama kubwa lakini makundi yote yakakubaliana, tofauti na ilivyo sasa kwa baadhi ya watu kwenda mahakamani na hii inaonyesha kuwa kuna tatizo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, “Mkutano huo una umuhimu mkubwa, ila ushauri wangu ni kuhakikisha kuwa pande zote zinakubaliana na kuwa kitu kimoja.” Dk Makulilo alisema kama washiriki wa mkutano huo watafikia mwafaka, makubaliano yao yanatakiwa kutoingilia utaratibu wa Bunge la Katiba wa kupiga kura kupitisha kifungu kwa kifungu, vinginevyo itakuwa ni kuingilia masuala ya kisheria.
“Katika hili napendekeza kuwa kitakachokubaliwa kitumike katika hatua zinazoendelea za kupata Katiba Mpya. Unajua mchakato ukiendelea kama ulivyo sasa bila mwafaka kupatikana Rasimu ya Katiba inaweza kukataliwa na wananchi katika kura ya maoni. Kwa sasa watu wanapinga mambo mengi yanayoendelea katika Bunge la Katiba,” alisema Makulilo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema hatua ya Rais Kikwete kukutana na makundi yaliyosusia kikao cha Bunge la Katiba ni mwafaka lakini kwanza Bunge hilo liahirishwe ili kupisha mazungumzo hayo.
Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea huku kukiwa na kikao cha kutafuta usuluhishi ni sawa na mtu anayejenga nyumba katika kiwanja chenye mgogoro.
“Kama umekubaliana na mwenzio kwamba tutakula chakula baada ya kumaliza mazungumzo, si sahihi mmoja aendelee kula mwingine akisubiri mazungumzo na ndicho wanachokifanya wajumbe wa Bunge la Katiba,” alisema na kuongeza kuwa Bunge hilo limepoteza dira na mwelekeo kutokana na viongozi wake kuanza kufanya kazi ya kukusanya maoni ambayo ilikwishafanywa na tume, kitendo alichosema kinaonyesha kuwa wameshindwa kuelewa mamlaka na majukumu ya chombo hicho. Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema licha ya uamuzi wa Rais Kikwete kuchelewa, mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa vile ndiyo yatakayosaidia kupata Katiba Mpya yenye maridhiano.
Mazrui alisema CUF itashiriki katika mazungumzo hayo ambayo yanasimamiwa na TCD chini ya Mwenyekiti wake, John Cheyo.
MWANANCHI


EmoticonEmoticon