Mafanikio ya Professor Muhongo Yaliza Watanzania Wengi



 professor Muhongo (Waziri Nishati na Madini)

UTEKELEZAJI wa shinikizo la kuvuliwa madaraka
kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, linaloendelea kutolewa na
wabunge na baadhi ya wanasiasa kwa Rais
Jakaya Kikwete, huenda ukaacha masononeko
kwa wananchi walionufaika na kipindi kifupi cha
uongozi wa waziri huyo.
Profesa Muhongo aliyejitengenezea uadui kwa
wafanyabiashara na wanasiasa, kutokana na
misimamo yake ya kulinda maslahi ya umma na
kuzungumza ukweli, huku akijiamini
kulikotafsiriwa kuwa ni dharau, hatima ya uongozi
wake ipo mikononi mwa Rais Kikwete, ambaye
ameshauriwa na Bunge kutengua uteuzi wake.
Katika azimio la saba, kati ya maazimio manane
ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
lililomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita,
kuhusu utoaji wa fedha katika akauti ya Tegeta
Escrow, iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), mamlaka ya uteuzi wa Profesa Muhongo,
imeshauriwa kutengua uteuzi huo.

Bunge linashauri na kuazimia Waziri wa Nishati
na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
wawajibishwe na mamlaka ya uteuzi itengue
uteuzi wao, limeeleza azimio hilo la saba.
Usambazaji umeme
Kama Rais Kikwete atatekeleza ushauri huo wa
Bunge na shinikizo la wanasiasa na
wafanyabiashara, uongozi wa muda mfupi wa
Profesa Muhongo takribani miaka miwili,
utakumbukwa kwa umahiri wa kusambaza
umeme vijijini.
Kabla ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo,
Watanzania asilimia 14 tu ndio waliokuwa
wakitumia nishati ya umeme, kati yao asilimia 12
walikuwa watumiaji wa mijini na asilimia mbili tu,
ndio walikuwa watumiaji wa vijijini.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, kati ya
mwaka 2007 na mwaka 2010, kulikuwa na
ongezeko la asilimia nne tu la watumiaji wa
umeme, hali iliyoonesha kuwa ongezeko la
Watanzania waliokuwa wakipata umeme, lilikuwa
asilimia moja kwa mwaka.
Lakini baada ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo
katika nafasi hiyo, katika muda mfupi wa uongozi
wake, idadi ya Watanzania wanaotumia umeme
iliongezeka na kufikia asilimia 36 katikati ya
mwaka huu.

Kwa hatua hiyo, uongozi wa Profesa Muhongo
ulivuka malengo ya Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ambayo ndio msingi wa
utekelezaji wa malengo ya Serikali, iliyotaka
Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, asilimia
30 ya Watanzania wawe wanapata umeme.
Baada ya kupita malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya
CCM, Profesa Muhongo aliamua kuweka malengo
mapya, ambapo alitarajia ifikapo 2015, asilimia
45 mpaka 50 ya Watanzania wawe na fursa ya
kutumia umeme.

Miongoni mwa Watanzania wanaokiri hilo ni
Diwani wa Kata ya Manga wilayani Tarime,
Omolo Ochola ambaye pia ni mchimbaji mdogo
wa madini kutoka Rorya.
Ochola alipozungumza na gazeti hili wiki hii,
alisema Waziri Muhongo amefanya kazi kubwa,
amesambaza umeme vijiji vingi hapa nchini na
kudhibiti ubadhirifu uliokuwepo hapo awali.
Mbali na Ochola, Mbunge wa Ntera, Livingston
Lusinde (CCM), alisema yeye hawezi kuona aibu
kuzungumzia mafanikio ya uongozi wa Profesa
Muhongo, huku akitoa mfano wa Tanesco kupigia
simu wateja ili ikawaunganishie umeme, kuwa
haikuwahi kutokea kabla ya uongozi wake.
Bei ya uunganishaji
Katika kutimiza malengo hayo, uongozi wa
Profesa Muhongo, ulitangaza punguzo la
gharama za kuunganisha umeme majumbani
kutoka Sh 177,000 za awali hadi Sh 27,000
vijijini.
Awali, punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya Lindi
na Mtwara, ambako bomba la kusafirisha gesi
kwenda Dar es Salaam limeanzia na limepita,
lakini baada ya muda gharama hizo zilishushwa
kwa vijiji vyote nchi nzima.
Profesa Muhongo mwenyewe alisema gharama
hizo zitahusu miradi inayosimamiwa na Wakala
wa Umeme Vijijini (REA), katika kipindi ambacho
wakandarasi watakuwa wakiendelea na awamu
ya pili ya miradi iiliyoanza Machi mwaka huu na
kutarajiwa kukamilika kati kati ya mwakani.
Profesa Muhongo alisema kuwa katika awamu ya
kwanza ya miradi iliyomalizika Desemba mwaka
jana, wanavijiji walilipa gharama kubwa, hivyo
uongozi wake uliamua kupunguza malipo hayo, ili
huduma hiyo ya nishati iwafikie watu wengi
zaidi.
Kufuta mgawo
Kuhusu suala la mgawo wa umeme, Profesa
Muhongo mwaka 2012 alisema mgao wa umeme
hautakuwepo tena na haukubaliki kamwe.
Profesa Muhongo alisema hadi Juni 2012 uwezo
wa mitambo ya kufua umeme (installed
capacity) ulikua megawati 1,375.74 (gesi asilia
ikiwa ni asilimia 40, maji asilimia 41 na mafuta
asilimia 19).

Alifafanua kuwa uwezo huo, ulikuwa ni ongezeko
la megawati 367 sawa na asilimia 36
ikilinganishwa na uwezo wa megawati 1,013.74
uliokuwepo Juni, 2011.
Alisema mahitaji ya juu ya umeme kwa mwaka
2011/12 yalifikia wastani wa MW 820.35
ikilinganishwa na MW 730 kwa mwaka 2010/11.
Tangu wakati huo, hakujatokea mgawo mkali wa
umeme kama uliotokea mwanzoni mwa mwaka
2011, na miaka ya nyuma ya hapo.

Tanzania kabla ya uongozi wa Profesa Muhongo,
ilikuwa ikikabiliwa na mgawo wa umeme wa
mara kwa mara, ambao mbali na kuathiri maisha
ya watu wa kawaida kutokana na kusababisha
mfumko wa bei, pia uliathiri sekta ya viwanda
ambapo baadhi vilitishia kufunga.
Kutokana na mgawo wa mara kwa mara,
mwanzoni mwa mwaka 2011, Shirikisho la Wenye
Viwanda Tanzania (CTI), liliwahi kutoa taarifa ya
kutishia kufungwa kwa viwanda 50 kati ya 280,
huku vingine vikitishia kupunguza uzalishaji,
kutokana na makali ya mgawo wa umeme.
Wamiliki hao walidai kupitia CTI kwamba, hawana
uwezo wa kutumia jenereta kwa ajili ya shughuli
za uzalishaji viwandani, kwa vile umeme wa
jenereta utawalazimu kulipia gharama za
matumizi ya nishati hiyo maradufu, tofauti na ile
inayozalishwa na Shirika la Umeme (Tanesco).
Walitoa mfano kuwa wakitumia umeme wa
Tanesco kwa kila kilowati moja, wanalipia senti
za dola ya Marekani nane mpaka tisa, lakini
wakitumia umeme wa jenereta, kwa kila kilowati
moja, wanatumia senti za dola ya Marekani 18
mpaka 20.
Mbali na hao, CTI ilieleza pia kuwa asilimia 15 ya
wanachama walitishia kuongeza bei ya kuuzia
bidhaa wanazozalisha na athari yake kwa
mapana, ilielezwa kuwa viwanda vitakosa
mapato, ajira kwa watumishi wa viwandani
zitapotea na Serikali pia itakosa mapato
yanayotokana na kodi za viwanda.
Aidha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilieleza
kuwa mfumko wa bei ulipanda na kufikia asilimia
6.4 kutoka asilimia 5.6, sababu kubwa ikiwa ni
mgawo wa umeme.

Ofisi hiyo ilitoa mfano wa bei ya vyakula na
vinywaji baridi, kwamba ilipanda kutoka asilimia
2.9 na kufikia asilimia 6.7 kutokana na mgawo
wa umeme.
Kushusha bei ya umeme Baada ya kufanikiwa
kufuta mgao wa umeme, kusambaza umeme kwa
wananchi na kuunganisha umeme kwa wananchi
kwa gharama nafuu, mwanzoni mwa mwaka huu,
Profesa Muhongo, alitangaza kusudio lake la
kushusha bei ya umeme.
Diwani Ochola wa Manga wilayani Tarime,
alisema Profesa Muhongo alikuwa amejiandaa
kushusha zaidi gharama za umeme mwakani.
Naye Musa Onyango, mchimbaji mdogo kutoka
Rorya, alisema gharama za umeme zilikuwa
zikipanda kila mwaka na kuwakatisha tama
Watanzania ikilinganishwa na kipindi cha mwaka
mmoja wa Profesa Muhongo ambapo kumekuwa
na ahueni kubwa ikilinganishwa na wakati wa
viongozi waliotangulia Kusudio hilo la kushusha
bei, lilitarajiwa kuanza kuonekana mara bomba la
gesi kufika jijini Dar es Salaam na mitambo ya
umeme kuanza kutumia gesi badala ya mafuta
mazito.

Uongozi wa Profesa Muhongo, uliweka wazi kuwa
wafanyabiashara wanaouzia umeme Tanesco,
wanauza uniti moja kwa kati ya Dola ya Marekani
senti 33 na 50.
Bei hiyo ya umeme kwa Tanesco kwa mujibu wa
takwimu za Serikali, ni kubwa kuliko bei ya
umeme ambayo shirika hilo linauza kwa
Watanzania wanaotumia umeme mdogo wa
majumbani, umeme wa kati kwa
wafanyabiashara, umeme wa kati wa viwandani
na umeme mkubwa kwa viwanda vikubwa, na
kubwa kuliko bei ya umeme ya mashirika ya
umeme ya nchi za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Takwimu za Tanesco, wateja wa
majumbani, uniti moja ya umeme wanauziwa kwa
dola ya Marekani senti 19, wateja wa biashara
senti 13 na viwanda vya kati na vikubwa senti
10.

Umeme wa taa za barabarani ni senti 19, wakati
Tanesco inanunua kwa senti 33 na 50. Profesa
Muhongo alisema bei ya umeme iliyopo, ni kwa
muda tu na itashuka sana bomba la gesi
likikamilika, kwa sababu hata mitambo ya kufua
umeme inayotumia mafuta nayo, itatumia gesi na
mitambo mipya ya gesi italetwa.
Alisema Serikali inataka umeme mwingi utokane
na gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo
wanaokataa bomba lisije Dar es Salaam na
nyuma yao, wapo wafanyabiashara ambao
wanahofia kuwa mwisho wa biashara yao ya
kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu umefika.
Msimamo huo wa Profesa Muhongo, uliwahi
kuungwa mkono na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
aliyesema mwishoni mwa Januari mwaka huu
alipokuwa Mtwara, kuwa Serikali imedhamiria
kuachana na umeme huo wa mafuta na kama
wafanyabiashara hao watataka kuendelea na
biashara hiyo, ni vyema wabadilishe mitambo yao
iwe ya gesi na sio ya mafuta kama ilivyo sasa
hivi.

Wataalamu wa gesi
Kutokana na ugunduzi mkubwa wa gesi
uliofanyika nchini, Profesa Muhongo pia
alianzisha utaratibu wa kusomesha Watanzania
wengi zaidi katika vyuo vya nje ya nchi katika
masuala ya gesi na mafuta, ili wananchi
wasimamie rasilimali hiyo kwa manufaa ya taifa
lao na vizazi vyao.
Lengo la Profesa Muhongo katika hilo, ni
kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kwanza
yenye wataalamu wengi wa mafuta na gesi,
katika nchi za bara la Afrika, baada ya miaka
mitano ijayo kwa kuwa na wataalamu zaidi ya
300 watakaokuwa wamesomea masuala hayo nje
ya nchi.
Pia amefanya juhudi kushawishi watanzania
ambao ni wataalamu mafuta na gesi zaidi ya 10
wanaofanya kazi nje ya nchi hususani nchini
Canada na Uingereza, mpaka wakakubali kurejea
kufanya kazi hizo nchini.

Utata wa kumwajibisha
Hatua ya Bunge kutaka Profesa Muhongo
awajibishwe, imetokana na maoni ya Mwenyekiti
wa Bunge wa Kamati ya Fedha za Serikali (PAC),
Kabwe Zitto, kuwa fedha hizo Sh bilioni 321 ni za
umma na utoaji wake na kwamba hatua ya
kulipwa kwa kampuni ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL), iligubikwa na harufu ya
ufisadi.
Hata hivyo, Profesa Muhongo katika utetezi
wake, alisema wakati wa kufunga akaunti hiyo
kulikuwa na Sh bilioni 182.77 tu, wakati deni
baada ya kupiga hesabu, lilikuwa Sh bilioni
275.20 na zote ni fedha za IPTL, zilizotokana na
mauzo ya umeme wake katika Shirika la Umeme
(Tanesco), na hivyo bado kampuni hiyo inaidai
shirika hilo la umeme Sh bilioni 123.90.
Mbali na kueleza kuwa kampuni hiyo ya IPTL
bado inaidai Tanesco, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Frederick Werema, ambaye naye
anatakiwa kuondolewa, alisisitiza kuwa akaunti
ya Escrow haikatwi kodi, ila kodi hiyo hukatwa
kwa mpokeaji wa fedha hizo na kutaka Mamlaka
ya Mapato (TRA), kwenda kudai kodi yake kwa
IPTL.
Profesa Muhongo na Werema mpaka sasa
msimamo wao ni kwamba fedha hizo si za
umma, huku Profesa Muhongo akisisitiza kuwa
mbali na kuwa si za umma, pia Serikali bado
inadaiwa Sh bilioni 123.90.
Lakini hata taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), hajathibitisha kuwa
fedha hizo ni za umma, bali ilieleza kuwa kuna
uwezekano kuwa katika fedha hizo, kuna fedha
za Tanesco, fedha za Serikali kwa maana ya
kodi na fedha za IPTL, ambazo ni mauzo ya
umeme kwa Tanesco.

Habari kwa Hisani ya Habari Leo.


EmoticonEmoticon